IQNA

OIC yataka misaada ifikishwe kwa Waislamu wa Myanmar

16:31 - August 18, 2012
Habari ID: 2395774
Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ametaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuwafikishia misaada Waislamu wa Myanmar wanaoendelea kuuawa na kunyanyaswa na serikali ya nchi hiyo.
Ametoa ujumbe wa kusaidiwa Waislamu hao kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Idul Fitr ambapo pia amewapongeza Waislamu wote duniani kwa kuwadia siku hii adhimu na ya furaha kwa umma wa Kiislamu.
Amesema, huku sehemu kubwa ya Waislamu wakijitayarisha kusherehekea sikuu hii sehemu nyingine za ulimwengu wa Kiislamu zinakabiliwa na matatizo na machungu mengi. Ameendelea kusema kuwa Waislamu wa Myanmar sasa wanakabiliwa na matatizo pamoja na vitendo vya mabavu ambavyo vinahatarisha maisha yao katika ardhi zao za jadi. Kwa msingi huo amewataka Waislamu wote ulimwenguni kujali na kuwazingatia wenzao wanaoteseka huko Myanmar na kuwafikishia haraka misaada ya kibinadamu.
Katibu Mkuu wa OIC ameutaka umma wa Kiislamu pia kuwajali ndugu zao wanaopata matatizo huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel na kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kulinda Quds Tukufu na utambuilisho wake wa Kiislamu na vilevile kuilinda kutokana na hujuma ya Mayahudi na Wazayuni.
Ihsanoglu amewataka Waislamu wawaunge mkono Wapalestina katika mapambano yao dhidi ya utawala haramu wa Israel hadi pale watakapofanikiwa kuunda nchi huru mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu. 1081522
captcha