Akihutubia katika mkutano wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini Yew York Marekani Rais Ahmadinejad amesema, mfumo wa kusimamia masuala ya dunia wa sasa ni wa kibaguzi na hauzingati uadilifu, hivyo dunia inahitajia fikra na mfumo mwingine mpya. Ameongeza kwamba, ili kuundwa mfumo huo nchi zote zinapaswa kushirikishwa katika kusimamia masuala mbalimbali ya kimataifa.
Dakta Ahmadinejad amesema, taifa la Iran kama ilivyo historia yake kongwe, lina fikra za kuisaidia dunia na linakaribisha jitihada na ushirikiano wa aina yoyote ile ili kuimarisha amani, usalama na utulivu. Amesisitiza kuwa maendeleo duniani yanayoweza kufikiwa tu kwa ushirikiano na usimamizi wa pamoja wa nchi zote. Aidha Rais Ahmadinejad amesema matatizo na migogoro ya dunia inaweza kutatuliwa kwa kuwepo nidhamu mpya ya kimataifa.
Amesema mashindano ya silaha na vitisho vya silaha za nyuklia na za mauaji ya umati yanayofanywa na nchi za Magharibi na Israel yamekithiri. Rais Ahmadinejad ameeleza kuwa, kuendelea vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel vya kulishambulia taifa la Iran ni mfano wa wazi wa ukweli huo mchungu.
Vilevile amekosoa vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini na kutusiwa Mitume wa Mwenyezi Mungu ambao ndio binadamu bora, kamili na waliotakasika zaidi. 1108119