IQNA

Intifadha ya Tatu ya Palestina inakaribia

22:17 - October 02, 2012
Habari ID: 2424761
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Palestina imeonya kuwa Intifadha ya tatu ya Palestina inakaribia kuibuka hivi karibuni kufuatia hujuma za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Mji wa Quds na Msikiti wa Al Aqsa.
Hayo yamedokezwa na Fawzi Barhoum msemaji wa Hamas ambaye amesema hali hivi sasa Palestina inashabihiana na ile iliyokuwepo wakati wa kuanza Intifahda ya pili.
Siku ya Ijumaa Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 wamefanya maandamano kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 12 wa Intifadha ya Quds.

Raia wa Palestina wanaoishi katika maeneo ya Shifa Amr, Al Nasra, Umul –Faham, Al Jalil na Al Muthalat huko katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1948 walifanya maandamano makubwa huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina na picha za mashahidi wa Intifadha ya Quds na kusisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni hadi kukombolewa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Waandamanaji hao wamelaani mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Kizayuni katika eneo la msikiti wa Al Aqsa mwaka 2000 na kwa mara nyingine tena wametaka kupandishwa kizimbani wale wote waliohusika na jinai hiyo. Tarehe 28 Septemba mwaka 2000 Ariel Sharon mmoja wa viongozi wa utawala wa Kizayuni huku akisaidiwa na vikosi vingi vya usalama na wanajeshi wa utawala huo alifanya kitendo cha kishenzi na cha kichokozi kwa kuingia ndani ya ua wa msikiti mtukufu wa al Aqsa. Kitendo hicho cha kifedhuli cha Wazayuni cha kuuvunjia heshima msikiti wa al Aqsa kiliibua hasira za raia wa Palestina na kuzusha mapigano kati yao na polisi wa Kizayuni, mapigano ambayo yalipelekea kuuliwa shahidi Wapalestina 13.

Msikiti wa al Aqsa ambao ni eneo takatifu la Kiislamu na kibla cha kwanza cha Waislamu una nafasi ya kipekee kwa Waislamu khususan Wapalestina. Na ndio maana Wapalestina na Waislamu duniani kote wanafuatilia masuala yote yanayohusu msikiti huo kwa hisia maalumu. Radiamali za Wapalestina kwa vitendo vya kujitanua vya utawala wa Kizayuni huko Baitul Muqaddas na pia hatua za kichokozi za utawala huo dhidi ya msikiti wa al Aqswa zinaashiria jinsi Wapalestina wanavyoendelea kuguswa na suala la Quds na juhudi zao zenye lengo la kulilinda eneo hilo takatifu la Kiislamu. Intifadha ya Quds inahesabiwa kuwa ni awamu ya pili baada ya Intifadha ya kwanza ya wananchi wa Palestina mwaka 1987, ambapo moja ya athari zake tangu ilipoanza katika mwaka 2000 ilikuwa ni kuipa sura ya kimataifa Intifadha ya wananchi wa Palestina.

Intifadha ya Quds imekuwa ikiuumiza kichwa na kuuyumbisha utawala ghasibu wa Kizayuni. Hii ni katika hali ambayo muqawama wa wananchi wa Palestina ulianza tangu utawala wa Kizayuni ulipoanza kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Hata hivyo kwa kushadidisha ukandamizaji wake dhidi ya raia wa Palestina utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa ukijaribu kila unaloweza ili kuwazuia Wapalestina wasiendeleze mapambano yao dhidi ya utawala huo ghasibu ili kwa njia hiyo uandae uwanja wa kuendeleza siasa zake za kujitanua huko Palestina, kuikalia kwa mabavu kikamilifu Baitul Muqaddas na kuubomoa msikiti mtukufu wa al Aqsa.

Hata hivyo wananchi wa Palestina siku zote wamekuwa wakionyesha kuwa kivyovyote vile hawatauruhusu utawala haramu wa Kizayuni utekeleze siasa zake hizo katika maeneo ya Palestina ikiwemo Baitul Muqaddas. Kuanza Intifadha ya Quds mwaka 2000 ikiwa ni radiamali kwa hatua za viongozi wa utawala wa Kizayuni za kuuvunjia heshima msikiti wa al Aqsa kunaashiria juu ya uhakika huo. Aidha kuendelezwa Intifadha dhidi ya siasa za utawala wa Kizayuni huko Quds kunaashiria azma ya wananchi wa Palestina katika kuyaunga mkono matukufu ya Kiislamu na kupigania haki yao ya kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu.

Katika fremu hiyo sambamba na kuadhimisha kutimia mwaka wa 12 tangu kuanza Intifadha ya Quds, harakati ya Mapambano ya Kiislamu Palestina Hamas imetoa taarifa na kusisitiza kuendelezwa muqawama dhidi ya Uzayuni kama njia pekee ya kuulinda msikiti wa Al Aqsa, matukufu ya Kiislamu na kurejesha haki za kisheria za Wapalestina zilizoghusubiwa na Wazayuni.

1112188
captcha