Akizungumza leo Jumatano hapa mjini Tehran wakati alipokutana na maelfu ya vijana wasomi bora na wenye vipawa vya juu nchini Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: ‘taifa la Iran kamwe halijawahi na halitasalimu amri mbele ya mashinikizo na hili ndilo jambo ambalo limewakasirisha maadui.’
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika kipindi cha miaka 33 iliyopita, pamoja na kuwepo mashinikizo mengi ya kisiasa, kiusalama, kijeshi, kiuchumi na vikwazo, taifa la Iran limesimama imara na si tu kuwa limesambaratisha mashinikizo hayo, bali pia limeweza kupata nguvu zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ulazima wa kutathminiwa ipasavyo uwezo na nguvu za mfumo wa Kiislamu, mashinikizo ya maadui na namna ya kuisambaratisha kambi hiyo ya maadui. Amesema dhana kuwa maadui walio katika kambi ya istikbari wanalishinikiza taifa la Iran kutokana na baadhi ya maamuzi yake si sahihi.
Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameongeza kuwa taifa la Iran kwa kutegemea utajiri wake wa kimaumbile na kibinaadamu litaweza kupita katika kipindi hiki kigumu na kwa taufiki yake Allah kuwasili katika kilele cha saada ya dunia na akhera sambamba na kupata utulivu na faraja. Ameendelea kusema kuwa sababu ya kubakia nyuma Iran kielimu katika miaka ya huko nyuma ni kuwepo watawala tegemezi na walioghafilika. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa pengo kubwa la kielimu na dunia pamoja na kuwepo ushindani mkubwa katika eneo ni ukweli ambao unaashiria udharura wa kuendelezwa maradufu harakati ya kasi ya ustawi wa kielimu hadi kufikia katika nafasi inayoistahiki taifa la Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema vijana wasomi na wenye vipawa ambao wana motisha kubwa katika harakati zao za ustawi wa kielimu wa Iran sasa wamegeuka na kuwa rasilimali ya taifa la Iran kwa faida ya wote.
1112919