IQNA

Katibu Mkuu wa OIC ataka misaada zaidi itumwe Somalia

23:08 - October 10, 2012
Habari ID: 2429577
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ametoa wito kwa nchi wanachama na jamii ya kimataifa kutuma misaada ya haraka nchini Somalia.
Profesa Ekmeleddin İhsanoğlu ametoa taarifa hiyo akiwa safarini mjini Mogadishu na huku akiashiria mabadiliko ya kisiasa yenye kutia matumaini nchini Somalia amesema kuwa, bado nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inahitaji misaada ya dharura.
Siku ya Jumanne İhsanoğlu alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mahmoud ambapo walijadili jinsi OIC inavyoweza kuisaidia Somalia. İhsanoğlu pia ametembelea kambi kadhaa za wakimbizi nchini Somalia.
Hivi karibuni mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga, alisema Somalia tayari imeshaanza kushuhudia mabadiliko muhimu, kufuatia chaguzi za bunge na rais zilizofanyika hivi karibuni nchini humo.
Balozi Mahiga alisema hali ya usalama mjini Mogadishu imeanza kuimarika na mitaa yake imeanza kushuhudia biashara na uwekezaji wa viwango vya juu. Mahiga amesema hivi sasa badala ya milio ya risasi, zinasikika sauti za nyundo za ujenzi katika mji huo mkuu wa Somalia.

1116449
captcha