Ombi hilo limetolewa kufuatia mashambulizi mapya yanayofanywa dhidi ya Waislamu huko magharibi mwa Myanmar ambayo yamesababisha vifo vya Waislamu zaidi ya 300. Duru za habari zimeripoti kuwa taasisi za jamii za Waislamu wa Rohingya kote duniani zimechapisha taarifa zikiitaka jamii ya kimataifa kuwazingatia Waislamu wa Myanmar na matatizo yao. Taarifa hiyo iliyosainiwa na makundi na taasisi kadhaa za kimataifa katika nchi kumi duniani imeitaka Kamisheni ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuwasaidia haraka Waislamu wa Rohingya huko Myanmar.
Serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu wa Rohingya kama raia wa nchi hiyo na inaamini kuwa watu hao ama wanapasa kuondoka nchini humo au kuishi kwenye kambi za wakimbizi. Hii ni katika hali ambayo tayari kuna baadhi ya kambi zilizoasisiwa katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Bangladesh zinazowahifadhi karibu wakimbizi 250,000 ambao walikimbilia katika kambi hizo miongo mitatu au minne iliyopita.
Kuendelea siasa za ubaguzi za serikali inayodai kufanya marekebisho huko Myanmar kumewafanya Waislamu wa nchi hiyo wakabiliwe na mashambulizi makubwa ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wanaoungwa mkono wa jeshi la nchi hiyo, mashambulizi ambayo yametajwa kuwa ni mauaji mapya ya kimbari. Serikali ya Myanmar imeifanya hali ya mambo ya nchi kuwa ngumu kwa kustafidi na hali hiyo iliyo dhidi ya ubinadamu ambayo imewalazimisha Waislamu kuikimbia nchi au kuelekea kwenye kambi za mpakani na zile zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuhofia kuuawa kwa umati na Mabudha wenye misimamo mikali. Hadi sasa mamia ya Waislamu wameuliwa katika mkoa wa Rakhine huko magharibi mwa Myanmar na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na upuuzaji wa serikali na kukaa kimya Umoja wa Mataifa na nchi zinazodai kutetea haki za binadamu ulimwenguni kuhusiana na ukatili huo.
Mashambulizi hayo dhidi ya Waislamu wa Rohingya yameibuka tena baada ya kusita kwa muda mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu. Vyombo vya habari vimetangaza kuwa zaidi ya Waislamu 300 wa Rohingya wameuliwa kwenye mapigano ya hivi karibuni huko magharibi mwa Myanmar na mamia ya wengine kuwa wakimbizi. Baadhi ya Waislamu wanaohofia maisha yao wamewasili katika mpaka wa Bangladesh na Myanmar kupitia njia za majini. Hata hivyo vikosi vya usalama vya Bangladesh vimekataa kuwaruhusu raia hao kuingia nchini humo. Viongozi wa Dhaka nao wamesema kuwa hawawezi kuwapokea wakimbizi hao. Ripoti zinasema kuwa wakimbizi wengi ambao wamepata hifadhi katika mikoa iliyoko kati ya Myanmar na Bangladesh wanaishi katika hali ngumu na wanakabiliwa na hatari ya kifo.
Zaidi ya Waislamu laki nane wa kabila la Rohingya wanaishi katika mkoa wa Rakhine na serikali ya Myanmar haiwatambui kuwa ni raia na wala hawapewi haki za kiraia au haki ya kumiliki. Waislamu hao ambao wamekuwepo Myamnar kwa zaidi ya miaka 1000 wanaitaka serikali ya nchi hiyo kukomesha dhulma za miaka mingi za serikali za kijeshi na kuwarejeshea haki zao za kiraia.
1134389