IQNA

OIC: Mauaji ya Waislamu wa Myanmar ni ya Kimbari

9:58 - November 18, 2012
Habari ID: 2450120
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC wamemaliza mkutano wao wa siku tatu nchini Djibouti Jumamosi hii ambapo wito umetolewa wa kuchukuliwa hatua za dharura kukomesha mauaji ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.
Mkutano huo ulioanza siku ya Alhamisi umejadili kwa kina mashambulizi ya jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Taarifa ya mwisho ya mkutano huo sambamba na kulaani jinai za Wazayuni huko Gaza, imezitaka nchi wanachama kuchukua hatua za kivitendo kukomesha jinai hizo. Pia wajumbe wamekubaliana kwamba OIC ipewe nafasi zaidi ya kushughulikia kadhia ya Syria. Jumuiya hiyo imepinga uingiliaji wowote wa kigeni katika mgogoro wa Syria na kusisitiza kwamba Wasyria wenyewe ndio watakaoweza kutatua mgogoro wao bila kushinikizwa na madola ya kigeni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mohammad Ali Yusuf ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho cha OIC ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo kukabiliana na mauaji ya Waislamu Myanmar. Naye Katibu Mkuu wa OIC Profesa Ekmeldin Ehsanoglu ametaka serikali ya Myanmar kuchukua hatua za haraka kustisha mauaji ya umati ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakine.
1139227
captcha