IQNA

Walimwengu waendelea kupinga jinai za Wazayuni huko Ghaza

16:05 - November 19, 2012
Habari ID: 2451296
Maandamano ya kuulaani na kutangaza hasira dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai zake yanaendelea katika kona mbalimbali za dunia.
Leo Jumatatu utawala wa Kizayuni wa Israel umeendeleza mashambulizi yake ya kikatili kwa siku ya sita mfululizo huku vyombo vya kimataifa na nchi zinazodai kutetea haki za binaadamu zikiendelea kunyamazia kimya na kufarijika na ukatili huo wa wanajeshi wa Israel. Walimwengu wakiwemo wa nchi za Ulaya, wanaendelea kuandamana wakitaka utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake huko Ghaza kama ambavyo wamezitaka pia nchi zao ziishinikize Israel ili iache mashambulizi yake hayo.
Mashinikizo ya walimwengu yamekuwa makubwa kiasi kwamba hata Jean-Claude MIGNON, mkuu wa Halmashauri ya Bunge ya Baraza la Ulaya imebidi atoe tamko akisema kuwa, jamii ya kimataifa haiwezi kukaa kimya na kuangalia kwa macho tu kutokea maafa mengine mapya huko Palestina.
Huko nchini Marekani nako baadhi ya wananchi wa nchi hiyo wameandamana mbele ya ikulu ya White House kulaani jinai za Israel huko Ghaza na kumtaka Barack Obama aonyeshe kivitendo kwamba ilikuwa ni haki yake kupewa tunzo ya amani ya Nobel.
Wanaharakati wa kijamii nchini Uingereza nao waliandamana hivi karibuni na kukusanyika mbele ya ubalozi wa utawala wa Kizayuni mjini London kulaani mashambulizi ya ndege za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Ghaza. Waandamanaji wanazihesabu serikali za Uingereza na Marekani kuwa zinashirikiana na utawala wa Kizayuni kufanya jinai za kivita huko Ghaza na kumtaka Rais wa Marekani arejeshe tunzo ya amani ya Nobel. Hata hivyo William Hague, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ameonyesha wazi jinsi madola ya kibeberu yanayozikingia kifua jinai za utawala wa Kizayuni. Si tu hakulaani jinai za Israel katika ukanda uliozingirwa wa Ghaza, lakini hata anathubutu kuwalaumu Wapalestina kutokana na kujitetea kwao mbele ya mawimbi ya mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni.
Mbali na Uingereza na Marekani, maelfu ya watetezi wa haki za binaadamu huko Ufaransa nako wameandamana kulaani jinai hizo za Israel. Inasemekana kuwa maandamano hayo ya nchini Ufaransa hayajawahi kutokea mfano wake kati ya maandamano ya kupinga utawala wa Kizayuni nchini humo.
Huko Ugiriki nako pia, wananchi wa nchi hiyo wameitisha maandamano ya kulaani jinai za Wazayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Nchini Austria pia wananchi wamefanya maandamano ya kuwatetea Wapalestina na kulaani jinai za Wazayuni.
Rais Vladimir Putin wa Russia amezungumza kwa njia ya simu na Rais Muhammad Mursi wa Misri akisisitizia haja ya kukomeshwa mara moja mashambulizi huko Ghaza.
Kiujumla ni kwamba madai ya utawala wa Kizayuni ya kwamba inafanya mashambulizi hayo ya kikatili dhidi ya wananchi wa Ghaza kwa ajili ya kujitetea hayawapumbazi tena walimwengu walio wengi ambao wanajua vyema kwamba Israel imejengeka juu ya misingi ya jinai na kumwaga damu za watu wasio na hatia. 1140308
captcha