IQNA

Rasimu ya katiba mpya ya Misri yapasishwa

11:39 - December 01, 2012
Habari ID: 2456239
Katika anga ya sasa ya vuta nikuvute nchini Misri, wanachama wa Baraza la Waasisi la nchi hiyo Alkhamisi walikutana na kujadili vipengee vya rasimu ya katiba mpya. Kikao hicho kilipasisha vipengee vyote 234 vya rasimu hiyo.
Sasa rasimu hiyo itapelekwa kwa Rais Muhammad Mursi kabla ya kupigiwa kura ya maoni ya wananchi.

Inatazamiwa kuwa hatima ya katiba mpya ya Misri itajulikana katika kipindi cha wiki mbili zijazo lakini suala muhimu zaidi kwa sasa ni hali ya mambo inavyoendelea nchini humo. Kwani katika upande mmoja hali ya mambo nchini inatokota kutokana na maamuzi ya wiki iliyopita ya Rais Mursi, na katika upande mwingine Mahakama ya Katiba ya Misri inatarajiwa kuitisha kikao tarehe Pili Disemba kujadili uhalali wa Baraza la Waasisi.

Awali mahakama hiyo ilitangaza kuwa baraza hilo si halali kutokana na kutohudhuriwa na robo ya wanachama wake. Hata hivyo wiki moja iliyopita Rais Muhammad Mursi alifuta maamuzi ya mahakama hiyo na kusisitiza kuwa maamuzi ya baraza hilo ni ya mwisho na kwamba yanapswa kutekelezwa.

Akitetea maamuzi yake ya hivi karibuni na hatua ya Baraza la Waasisi ya kupasisha rasimu ya katiba mpya, Mursi amesema kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa shabaha ya kuharakisha mwenendo wa kisiasa nchini.

Waungaji mkono wa kiongozi huyo wanasema, kukamilishwa uchunguzi wa rasimu ya katiba mpya ni hatua ya kwanza katika njia ya kurejesha utulivu na amani kamili nchini Misri. Hata hivyo hatupasi kusahau kuwa Misri inapita katika kipindi nyeti na muhimu. Jamii ya nchi hiyo pia inajumuisha makundi yenye mitazamo na mirengo mbalimbali ya kisiasa. Kwa msingi huo harakati na msimamo wa kundi lolote lile katika mazingira ya sasa huwa kama cheche ya moto katika ghala la baruti. Vilevile tunapaswa kuelewa kuwa matukio ya hivi karibuni nchini Misri yametayarisha uwanja mzuri kwa makundi yanayopinga mapinduzi ya wananchi yaliyoung'oa utawala wa kidekteka wa Hosni Mubarak.

Wakati huo huo baadhi ya wapinzani wa kisiasa wa Mursi wametumia mazingira yaliyojitokeza baada ya kutangazwa maamuzi yake ya hivi karibuni na kumtuhumu kiongozi huyo kuwa ametupilia mbali malengo ya mapinduzi ya wananchi.

Ni wazi kuwa anga ya ndani ya Misri imekuwa medani ya mpambano baina ya waungaji mkono na wapinzani wa Rais wa nchi hiyo. Ni kawaida kwamba katika anga kama hiyo soko la tetesi na uvumi hupata wanunuzi wengi na kila hatua au mtazamo wa viongozi wa serikali na asasi za kisiasa hufasiriwa visivyo na makundi mbalimbali ya upinzani.

Katika hali hii kuna udharura kwa Wamisri kuwa macho na kutambua kwamba, umoja wao wa kitaifa unakabiliwa na hatari kubwa na iwapo mantiki na busara haitatawala haraka, basi kuna uwezekano mkubwa wa matunda ya mapinduzi ya wananchi yakasombwa na kimbunga cha machafuko na hitilafu za mirengo mbalimbali ya kisiasa.
1145469
captcha