IQNA

Imam Khamenei: Iran haitosalimu amri mbele ya ubabe wa Marekani

20:48 - February 17, 2013
Habari ID: 2498007
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema maandamano ya kila mwaka ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mithili ya dharba nzito inayowashukia maadui na wapinzani wa taifa la Iran na kusisitiza kwamba mwaka huu pia hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumamosi alipokutana na mjumuiko mkubwa sana wa maelfu ya wananchi wa Tabriz (makao makuu ya mkoa wa Azerbaijan Mashariki wa kaskazini magharibi mwa Iran). Katika hotuba yake muhimu sana alifafanua kuhusu maneno na matendo yasiyo ya kimantiki ya viongozi wa Marekani kuhusiana na madai yao ya kutaka mazungumzo na Iran na pia amebainisha muamala wa kimantiki wa taifa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala hilo na kwa mara nyingine amewashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi na kwa ghera kubwa katika maandamano ya Siku ya Mwenyezi Mungu yaani Bahman 22 (zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran), kama ambavyo pia amezungumzia tukio la hivi karibuni lililotokea kwenye Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran.
Katika mkutano huo ambao umefanyika kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya mapambano ya wananchi wa Tabriz ya tarehe 29 Bahman 1356 (Hijria Shamsia sawa na Februari 18, 1978), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbuka kwa kheri mashahidi wa mapambano hayo na kusema kuwa, dini na imani ya kidini ndivyo vielelezo, vipimo, dira na vienzo vya harakati ya taifa la Iran.
Ameongeza kuwa, mfano wa wazi wa uhakika huo ni mapambano ya wananchi wa Azerbaijan katika kipindi cha miaka 150 iliyopita ambao katika kipindi chote hicho waliifanya imani ya dini na kushikamana na mafundisho ya dini yao kuwa ndiyo nguzo ya kutegemea.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia juu ya uhakika kwamba imani ya kidini ya taifa la Iran ndiyo sababu kuu iliyolifanya taifa hili kutotetereka mbele ya mashinikizo ya madola ya kibeberu duniani ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kila namna vya madola hayo na kuongeza kuwa, mabeberu hao katika miezi kadhaa iliyopita waliliwekea taifa la Iran vikwazo vipya ambavyo walidai kuwa vinalenga kulifanya kilema taifa hili na hata siku chache kabla ya maadhimisho ya Bahman 22 (siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran), waistikbari waliweka vikwazo vipya dhidi ya taifa la Iran ili kuwafanya wananchi wa taifa hili walegeze kamba na wasitesite katika mambo na misimamo yao, lakini majibu ya taifa la Iran yalionekana wazi kwenye maandamano ya Bahman 22 ya mwaka huu ambayo yalikuwa ya kufana, makubwa na ya hamasa kubwa zaidi kuliko miaka iliyopita.
Ameongeza kuwa: Katika maandamano ya Bahman 22 mwaka huu, watu wote walishiriki kwenye maandamano hayo kutoka pande zote. Wananchi walishiriki kwenye maandamano hayo kwa mori wa hali ya juu wakiwa na nyuso za bashasha na tabasamu na kwamba kwa mara nyingine madhuhurio hayo adhimu yameonyesha sura halisi ya taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwamba, kama ambavyo maandamano ya Bahman 22 kila mwaka hutoa pigo kubwa kwa maadui na wapinzani wa taifa la Iran, mara hii pia hali ilikuwa vivyo hivyo.
Vile vile kwa mara nyingine amewashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika maandamano ya Bahman 22 na kusema kuwa: Hata kama tutashukuru mara mia moja bado tutahitajika kuwashukuru tena na tena wananchi kwa moyo na muono wao wa mbali waliouonesha katika maandamano hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amezungumzia kiuchambuzi hali iliyopo hivi sasa na kusisitiza kuwa: Maadui wako katika hali mbaya hivi sasa mbele ya imani, nia na azma ya kweli, tabasuri na muono wa mbali, ushujaa na uvumilivu wa taifa la Iran na ni kwa sababu hiyo ndio maana wanafanya mambo yasiyo ya kimantiki na yasiyoingia akilini.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi kwenye matendo na maneno ya viongozi wa Marekani na kusema kuwa, viongozi hao si watu wa mantiki, ni watu wenye maneno yanayokinzana na matendo yao, na ni watu wenye roho za kupenda kuyakandamiza mataifa mengine.
Ameongeza kuwa: Wamarekani wanataraji kuwaona watu wengine wakisalimu amri mbele ya maneno yao ya kibeberu yasiyoingilika akilini, kama ambavyo baadhi ya watu wamebwaga manyanga na kusalimu amri mbele ya uistikbari wao. Lakini taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kamwe hauwezi kubwaga silaha na kusalimu amri mbele ya ubeberu wa Wamarekani kwani taifa na mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini Iran unatumia mantiki, una uwezo na una nguvu.
Huku akibainisha misimamo na vitendo visivyo vya kimantiki vya viongozi wa Marekani na serikali za nchi za Magharibi zinazoifuata kibubusa Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mifano ya wazi ya jambo hilo akisema kuwa: Viongozi hao wanadai kuwa wanaheshimu haki za binaadamu na ni viranja wa kupigania haki za binaadamu duniani. Lakini katika vitendo ni wao waliotoa pigo kubwa sana kwa haki za binaadamu na ni wao ndio waliofanya maafa makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa mfano wake huko Guantanamo, Abu Ghureib na hadi leo wanaendelea kuwaua wananchi wa Afghanistan na Pakistan na kukanyaga vibaya sana haki za binaadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja jambo jengine linaloonesha kuwa matendo na maneno ya Wamarekani yanakinzana na si ya kimantiki kuwa ni madai yao kwamba, wanapambana na silaha za nyuklia.
Amesema: Miaka 11 iliyopita Wamarekani waliivamia Iraq kwa madai hayo hayo lakini baadaye ilikuja kuthibitika kuwa madai ya Wamarekani kuhusu Iraq yalikuwa ni uongo mtupu.
Vile vile amesema, viongozi wa Marekani wanajigamba kupambana na silaha za nyuklia katika hali ambayo wanauunga mkono kwa kila hali utawala mshari na katili wa Kizayuni na kuuzatiti kwa silaha za mauaji ya umati za nyuklia ambazo zinatumika kuyatisha mataifa mengine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameyataja madai ya Wamarekani ya kuwa wanaheshimu demokrasia na wanapigania demokrasia duniani kuwa ni maneno mengine yasiyo ya kweli na kuongeza kuwa: Wamarekani kwa upande mmoja wanadai kutetea demokrasia lakini kwa upande wa pili siku zote wanaipinga Iran na kusimama dhidi yake wakati Iran ndiyo nchi yenye mfumo wa wazi na wadhiha kabisa wa demokrasia katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Wamarekani wanadai kuwa wanalinda na kupigania kuenea demokrasia duniani wakati katika eneo hili hili la Mashariki ya Kati wanaziunga mkono kwa jeuri kubwa nchi ambazo hazijawahi kunusa hata harufu ndogo tu ya demokrasia na wananchi wa nchi hizo hawajawahi hata mara moja kwenda kwenye masanduku ya kupigia kura.
Ametaja mfano mwingine wa wazi wa kuweko migongano kati ya maneno na matendo ya viongozi wa Marekani kuwa ni madai yao ya kwamba wako tayari kufanya mazungumzo na Iran kwa ajili ya kutatua masuala yaliyopo baina ya nchi hizi mbili.
Amesema: Madai hayo yametolewa katika hali ambayo Wamarekani wanaendelea kutoa matamshi yasiyostahiki kutolewa na yaliyo kinyume na ukweli na kuyanasibisha na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wanatumia vikwazo na mashinikizo kwa ajili ya kukabiliana na taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria, matamshi ya siku chache zilizopita ya Rais wa Marekani aliyedai kuwa nchi yake inafanya juhudi za kuizuia Iran isitengeneze silaha za nyuklia na kusisitiza kuwa: Kama Iran ingelikuwa na nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, Marekani kamwe isingelikuwa na uwezo wa kulizuia taifa la Iran kufanya hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia na uamuzi huo imeuchukua si kwa sababu ya kutaka Marekani isikasirike, bali ni kutokana na imani na itikadi yake ya kidini inayosisitiza kwamba kutengeneza silaha za nyuklia ni jinai dhidi ya mwanadamu na ndio maana inasisitizia pia haja ya kutotengenezwa kabisa silaha hizo za mauaji ya umati na inataka silaha zote za nyuklia zilizopo duniani leo ziangamizwe.
Vile vile amesisitiza kuwa: Madai ya Wamarekani kwamba Iran inataka kutengeneza silaha za nyuklia ni kupotosha maneno.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kadhia ya nyuklia ya Iran haina uhusiano kabisa na suala la kutengeneza silaha za nyuklia, bali nchi za kibeberu zinataka kulizuia taifa la Iran lisitumie haki yake ya wazi ya kurutubisha urani na kutumia nishati hiyo muhimu kwa njia za amani wakati hiyo ni haki ya kila nchi duniani.
Amesema: Tab'an watashindwa tu katika njama zao za kulizuia taifa la Iran kustafidi na teknolojia hiyo na kwamba taifa hili litastafidi vizuri na haki yake hiyo iliyo wazi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Njama za kutaka kulinyima taifa la Iran haki yake ni mfano mwingine wa wazi wa kutokuwa na mantiki viongozi wa Marekani na ni kwa sababu hiyo ndio maana tukasema kuwa haiwezekani kuwaamini na kuwa na matumaini na watu ambao wanatumia mabavu na kutokuwa na mantiki katika matamshi na matendo yao.
Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote hiki cha miaka 34 iliyopita imefahamu vyema - kupitia anga mbali mbali za kimataifa - iamiliane vipi na upande inaokabiliana nao kwani inajua vizuri matendo yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kuwa, Wamarekani wanafanya njama za kuwadanganya walimwengu kupitia kanali za habari zinazomilikiwa na Wazayuni na Wamarekani na kuongeza kuwa: Kanali za kimataifa za habari imma haziakisi maneno yetu au zinaakisi nusu bali hata wakati mwingine zinaakisi kinyume kabisa na tunavyosema, hivyo matamshi yangu hapa yanalilenga taifa la Iran.
Vile vile amesisitizia nukta tano muhimu katika kubainisha matukio na kadhia mbalimbali zinazohusiana na mazungumzo kati ya Marekani na Iran ambayo ni kutokuwa ya kimantiki na kugongana maneno na matendo ya viongozi wa Marekani, njama za Wamarekani za kutaka kulifanya taifa la Iran lisalimu amri na hilo ndilo lengo lao kuu la kupendekeza mazungumzo hayo, maana hasa ya neno mazungumzo mbele ya madola ya kibeberu, uongo na hila za Wamarekani kuhusiana na kuondoa vikwazo kupitia mazungumzo na kuwa wa kimantiki msimamo wa taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu pendekezo la mazungumzo lililotolewa na Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja lengo kuu la viongozi wa Marekani la kutoa pendekezo la mazungumzo na Iran ni kufanya poropaganda na kueneza uvumi kwenye mabanda yao ya kueneza propaganda ili kujaribu kuonesha kwamba taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hatimaye umesalimu amri na sasa unataka mazungumzo na Marekani na kuongeza kuwa: Wamarekani wanataka kuyaonesha mataifa ya Waislamu na yale yaliyoamka katika eneo hili kuwa hata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hatimaye imeburuzwa kwenye meza ya mazungumzo na mapatano licha ya kusimama kidete kwa muda mrefu, hivyo na nyinyi mataifa mengine ya Kiislamu nanyi hamna njia nyingine isipokuwa kusalimu amri mbele yetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kwa kusisitiza kuwa: Tab'an kwa muda mrefu madola ya kibeberu yamekuwa yakifanya njama za kuyakatisha tamaa mataifa ya Waislamu kupitia kuiburuza Iran kwenye meza ya mazungumzo na hadi leo hii wanaendelea na njama zao hizo kupitia kuendesha propaganda za kufanya mazungumzo juu ya masuala yasiyo ya kimsingi, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko macho na inayaelewa vizuri malengo yao na inatoa majibu yake kulingana na malengo hayo ya mabeberu.
Amesema kuwa, maana ya kweli ya mazungumzo kwa mtazamo wa Marekani na Wamagharibi ni kukubaliana na maneno yao tu katika meza ya mazungumzo na kusisitiza kuwa: Wamagharibi wamekuwa wakifanya propaganda nyingi katika siku za hivi karibuni kwa kutumia mtazamo wao huo huo usio wa kimantiki na usioingia akilini wakidai kuwa wako tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran ili Iran iachane na masuala yake ya nyuklia na kurutubisha urani lakini kama Wamagharibi wangelikuwa wanataka mazungumzo ya kweli na ya kimantiki basi wasingelisema hivyo bali wangelisema tunataka kuzungumza na Iran tuweze kusikia tusikie hoja na msimamo wa Iran ili kwa njia hiyo tuweze kuchanganua masuala husika kwa njia za kiadilifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amehoji akisema kwamba kwa vile Wamarekani wanatawaliwa na fikra kama hizo na wanachosubiri wao ni kuona Iran inasalimu amri, je, kutakuwa na faida yoyote ile kwa serikali ya Iran kukubaliana na pendekezo lao la mazungumzo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria tabia ya Wamarekani ya kukwamisha mazungumzo wakati wanaposhindwa kwenye mazungumzo hayo na baada ya kukosa hoja mbele ya maneno ya kimantiki ya Iran na kuongeza kuwa: Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, mara mbili au tatu hivi Wamarekani walisisitiza kuwa mazungumzo na Iran ni jambo la dharura, ni muhimu na ni suala ambalo inabidi lifanyike haraka sana kuhusu baadhi ya masuala. Afisa mmoja au maafisa wawili hivi wa serikali ya Iran wakaenda kufanya mazungumzo nao lakini ya Wamarekani baada ya kusikia maneno ya kimantiki ya Iran na kushindwa kutoa majibu sahihi, ghafla walikwamisha mazungumzo hayo na wakatumia vyombo vyao vya habari vya kimataifa kujaribu kuonesha kuwa Iran ndiyo iliyokwamisha mazungumzo hayo.
Vile vile ameuliza swali kwamba je, kwa kuwepo uzoefu wote huo, bado kuna haja ya kuyajaribu tena maneno yasiyo ya kimantiki ya Wamarekani kwenye meza ya mazungumzo?
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amezitaja propaganda za Wamarekani kuhusu kuiondolea vikwazo Iran kama itakubali kufanya mazungumzo kuwa ni ahadi za uongo na kuongeza kwamba: Kwa fikra zao pumba, Wamarekani wanadhani kuwa, wananchi wa Iran wamefika mwisho wa njia kutokana na vikwazo vyao hivyo walivyowawekea na kwamba watakaposikia ahadi hizo watafanya haraka kwenda kwenye meza ya mazungumzo kwa shauku kubwa na watawashinikiza viongozi wao kufanya hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kwa kweli ahadi hizo nazo ni mithili ya maneno yale yale ya kidanganyifu ya Wamarekani na zinaonesha kuwa Wamarekani hawataki mazungumzo ya kweli na ya kiadilifu, bali wanachotaka wao ni kuona wananchi wa Iran wanasalimu amri wakati ambapo kama wananchi wa Iran wangelitaka kuwa chini ya udhibiti wa Wamarekani basi wasingelifanya mapinduzi kabisa (yaliyomfukuza Mmarekani nchini Iran).
Aidha ametaja tatizo jingine kubwa linaloonekana kwenye madai ya Wamarekani kuhusiana na kuiondolea vikwazo Iran kama itakubali kufanya mazungumzo kuwa ni uhakika kwamba lengo la vikwazo hivyo kama ambavyo amesema mara nyingi ni kuwachosha wananchi wa Iran na kuwafanya wajitenge na mfumo wao wa Kiislamu. Hivyo kama mazungumzo hayo yatafanyika, lakini wananchi wa Iran nao wakaendelea kuwepo kwenye medani ya kutetea haki zao kwa nguvu zao zote, bila ya shaka yoyote Marekani nayo itaendelea kuwawekea vikwazo wananchi hao.
Vile vile amezungumzia mtazamo fulani wa Wamarekani na kusema kuwa nusu ya mtazamo wao huo ni sahihi na nusu nyingine ni ghalati.
Amesema: Wamarekani wanaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu inategemea wananchi na kama watatumia vikwazo kuwatenganisha wananchi wa Iran na mfumo wa Kiislamu, basi nguvu za muqawama na mapambano za Jamhuri ya Kiislamu zitapotea. Sehemu ya awali ya maneno hayo kwamba mfumo wa Kiislamu wa Iran unategemea kikamilifu wimbi adhimu la wananchi ni maneno ya kweli lakini sehemu ya pili kwamba vikwazo na mashinikizo yatawapigisha magoti wananchi wa Iran na kuwafanya wajitenge na mfumo wa Kiislamu ni maneno ghalati kikamilifu na yanatokana na welewa mbaya walio nao Wamarekani kuhusiana na wananchi wa Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an wananchi wa Iran wanataka ufanifu, ujazi na ustawi uliokamilika lakini pia hawako tayari kufikia lengo hilo kwa idhilali na kudunishwa bali wanataka wapate mafanikio hayo kwa tadibiri, uchapaji kazi na ushujaa na kwa kutegemea nguvu zake za ndani hasa vijana wa Iran wenye vipaji vingi na walio laiki kufanya mambo makubwa makubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia maendeleo ya kustaajabisha liliyoyapata taifa la Iran ikilinganishwa na wananchi wa mataifa na nchi nyingine zilizokubali kuwa chini ya udhibiti wa Marekani na kuongeza kuwa: Ni kweli vikwazo vinawasumbua wananchi lakini katika kukabiliana na vikwazo hivyo hakuna njia zaidi ya mbili; imma kutubu na kusalimu amri mbele ya mabeberu wa dunia kama yanayofanya mataifa dhaifu, au kuwa kama lilivyo taifa shujaa la Iran; kupambana kiume na vikwazo hivyo kwa kuzidisha uwezo na nguvu zake za ndani na kuvuuka kifua mbele na kwa ufakhari na nguvu kubwa katika kipindi hiki kilichojaa hatari.
Ameongeza kuwa: Bila ya shaka yoyote taifa la Iran limechagua njia hiyo ya pili na litaendelea kuwa na msimamo huo na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu litabadilisha vikwazo hivyo kuwa fursa ya ustawi na kujiletea maendeleo makubwa zaidi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameitaja hatua ya wananchi wa Iran ya kushiriki kwa wingi mno kwenye maandamano ya Bahman 22 (ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) kwamba haina maana kuwa wananchi hawaumizwi na ughali wa maisha au hawaulalamikii ugumu huo wa maisha na kuongeza kuwa: Wananchi na hasa wa matabaka dhaifu na ya chini wanahisi uzito kikamilifu katika maisha, lakini pamoja na hayo wameshikamana vilivyo na mfumo wao wa Kiislamu kwani wanajua kuwa mfumo huo wa Kiislamu na dini tukufu ya Kiislamu ndiyo nguvu pekee yenye uwezo wa kuwatatulia matatizo yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa hotuba yake kuhusu mazungumzo na Marekani akisisitiza kuwa: Mfumo wa Kiislamu na taifa la Iran - tofauti na walivyo Wamarekani - ni mfumo na ni taifa linalofuata mantiki, hivyo linapokutana na upande unaofuata mantiki, nalo hutoa majibu yake kulingana na mantiki ya upande huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, viongozi wa Marekani wanapaswa kuonesha nia njema kwa taifa na wananchi wa Iran. Ametaja baadhi ya dalili za nia hiyo njema kuwa ni kuachana Marekani na taiba yake ya ubeberu na ushari, kuheshimu haki za taifa la Iran, kutoingilia masuala ya ndani ya Iran kama ilivyofanya katika kuunga mkono fitna ya mwaka 2009 iliyosababisha machafuko mjini Tehran na kuacha kueneza fitna na machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati. Amesema kama dalili hizo zitaonekana basi Iran itahisi kuwa viongozi wa Marekani wameonesha nia njema.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama hali itakuwa hivyo na Wamarekani watathibitisha kwa maneno na kwa vitendo kuwa ni watu wa mantiki na wanaofanya mambo yanayoingia akili, hapo wataona kuwa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran kuwa nalo ni lenye kupenda mambo ya kheri na ni la kimantiki linalopenda sana ushirikiano.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuamiliana kwa njia sahihi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni kwa njia hiyo ndipo serikali ya Marekani itapata majibu mazuri kutoka Iran.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia suala muhimu lililotokea siku ya Jumapili ya wiki mbili zilizopita katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kuzungumzia nukta muhimu kuhusu kadhia hiyo.
Kiongozi Muadhamu amegusia jinsi wananchi na watu muhimu katika jamii walivyosikitishwa na jambo hilo na kuongeza kuwa: Mimi pia nimesikitishwa mara mbili na jambo hilo baya na lisilofaa. Upande mmoja nimesikitishwa kwa kuona kuwa jambo hilo limetokea na upande wa pili nimeumia kwa kuona jinsi wananchi walivyoumizwa na jambo hilo.
Ameongeza kuwa: Inasikitisha kuona kuwa katika kadhia hiyo, mkuu wa mhimili mmoja wa dola alitegemea tuhuma ambazo hazijathibitishwa bali hata hazijafikishwa mahakamani kutoa tuhuma dhidi ya mihimili mingine mikuu ya dola yaani Bunge na Mahakama jambo ambalo ni baya, ni ghalati na si sahihi, ni kinyume cha sheria na ni kinyume na maadili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kitendo hicho kimewavunjia pia wananchi haki zao za kimsingi kwani kuishi katika utulivu na usalama wa nafsi na maadili ni miongoni mwa haki za kimsingi za taifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Hivi sasa mimi ninatoa nasaha kuwa kitendo hiki si kizuri hata kidogo kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Vile vile amesema kitendo cha Bunge nacho cha kumwita waziri kumsaili Bungeni lilikuwa ni kosa na kuongeza kuwa: Kumwita mtu bungeni inabidi kuwe na faida. Lakini wakati miezi michache tu imebakia hadi kumalizika wakati wa serikali iliyopo madarakani, kwenda kumwita Bungeni Waziri tena basi kwa jambo ambalo hata yeye hahusiki nalo kuna sababu na faida gani?
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema, ndani ya Bunge pia kuna watu walitoa maneno yasiyo sahihi jambo ambalo ni kosa na ni ghalati.
Aidha amesema jinsi Mheshimiwa Spika naye alivyojitetea pia kwa kiasi fulani kulikuwa na kuchupa mipaka na kwamba alisema mambo ambayo hayakuwa na haja ya kusemwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Yote yaliyofanyika hayakuwa sahihi, si zile tuhuma zilizotolewa, si namna watu walivyoamiliana na tuhuma hizo Bungeni na si uitaji wenyewe wa Waziri Bungeni, yote hayakuwa sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameuliza swali akisema: Wakati pana adui wa pamoja na kuna njama za kila namna zinalielekea taifa kutoka kila upande, hivi kweli kuna haja ya kufanyika jambo jingine ghairi ya kuongeza udugu na mshikamano katika kupambana na adui?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia jinsi anavyowaunga mkono viongozi nchini na kuongeza kuwa: Mimi nitaendelea kuwaunga mkono viongozi, lakini vitendo kama hivi havioani na viapo na ahadi walizotoa. Viongozi wanapaswa kuuona uadhama wa taifa na kufanya mambo mazuri linayostahiki kufanyiwa taifa kama hili.
Amesisitiza pia kuwa, viongozi, Serikali, Bunge na watu wote wanapaswa kuhakikisha wanalenga juhudi zao zote katika kutatua matatizo ya kiuchumi ya wananchi na ya nchi kwani kama alivyosema miaka kadhaa iliyopita kuwa, adui amelenga njama zake upande wa masuala ya kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Miaka kadhaa iliyopita niliwatumia barua wakuu wa mihimili mikuu ya dola kuhusiana na kupambana na ufisadi wa kiuchumi na kwa mara nyingine ninasema hapa kuwa haiwezekani kupambana na ufisadi wa kiuchumi kwa maneno matupu, bali kunahitajika mapambano ya kivitendo, sasa katika vitendo kumefanyika nini? Mumefanya nini katika vitendo? Mtu akifikiria jambo hili anaumia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Taqwa! Taqwa! Taqwa! Tunachotarajia kuona kutoka kwa viongozi ni subira, kutoingiza masuala ya hisia katika medani na kutoyapa umuhimu mambo binafsi katika masuala ya nchi. Tunachotarajia ni kuona viongozi wanatumia nguvu zao zote kutatua matatizo ya wananchi. Hivi sasa ambapo uadui wa maadui umeongezeka sana, wanachopaswa kufanya viongozi si kitu kingine ila na wao kuzidisha urafiki na mapenzi baina yao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inshaallah nasaha hizi za kutaka kheri na zilizojaa huruma wazizingatie viongozi hususan viongozi wa juu na washikamane nazo.
Amesisitiza pia kuwa: Tab'an sitarajii kuona kwamba masikitiko yangu haya ya leo kuhusiana na vitendo vya baadhi vya viongozi yatapelekea baadhi ya watu waanze kutoa maneno mabaya dhidi ya viongozi hao, mimi ninapinga jambo hilo.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepinga vikali na waziwazi kitendo cha hivi karibuni kilichofanywa na baadhi ya watu waliovuruga hotuba ya Spika wa Bunge mjini Qum na kuongeza kuwa: Kitendo cha baadhi ya watu kuwaita wenzao kuwa wako dhidi ya "Wilaya" na dhidi ya tabasuri na muono wa mbali kama ilivyotokea hivi karibuni huko Qum, ni kitendo ghalati na mimi ninapinga kikamilifu vitendo kama hivyo ambavyo mfano wake viliwahi kutokea pia katika Marqad tukufu ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh) na niliwatahadharisha viongozi nikiwataka wasiruhusu kutokea mambo kama hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Watu wanaoibuka na kuanza kutoa maneno kama hayo kama kweli ni watu walioshikamana vilivyo na dini na ni waumini wa kweli basi wajue kuwa mambo hayo yana madhara kwa nchi na ni kinyume cha sheria au lau kama hawajali maneno haya basi hesabu ya watu hao ni nyingine.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, mustakbali wa taifa lenye muono wa mbali la Iran ni mzuri kikamilifu na kwa kweli mustakbali bora zaidi na unaong'ara zaidi unalisubiri taifa na vijana wa nchi hii.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Muhammad Mujtahid Shabistari, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala mkoani Azerbaijan Mashariki ambaye pia ni Imam wa Ijumaa wa mji wa Tabriz ametoa hotuba fupi na sambamba na kuwakumbuka kwa kheri mashahidi wa harakati ya Bahman 29, 1356 (Hijria Shamsia sawa na Februari 18, 1978 Milaadia), ameashiria jinsi wananchi wa Iran walivyoshiriki kwa wingi sana katika maandamano wa Bahman 22 mwaka huu (Februari 10, 2013, zilipofikia kileleni sherehe za miaka 34 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) na kusema kuwa: Ujumbe wa wananchi wenye muono wa mbali wa Iran ambao wanazijua vyema zama na nyakati katika maandamano hayo ya aina yake ya Bahman 22 ni kulindwa umoja na mapenzi katika jamii na kuzingatia maadili mazuri katika uga wa kisiasa na viongozi kufanya jitihada maradufu za kutatua matatizo ya wananchi.
1189406
captcha