IQNA

Shule za Kiislamu zafanya vizuri Uingereza

10:05 - February 26, 2013
Habari ID: 2502605
Shule za Kiislamu nchini Uingereza zimetajwa kuwa ni miongoni mwa shule bora kwenye orodha za taasisi za kielimu nchini humo, baada ya wanafunzi wa shule hizo kufanya vyema kwenye masomo yao.
IQNA imemnukuu Hamid Patel Mkuu wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya 'Tawhidul Islam' akisema kuwa, wanafunzi Waislamu nchini Uingereza wanafanya vizuri kwenye masomo yao licha ya kukabiliwa na matatizo mengi. Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tawhidul Islam iliyoko katika mji wa Blackburn pamoja na shule nyingine, zimeongoza kwenye orodha ya shule zilizofanya vizuri kimasomo katika mji huo. Takwimu zilizotolewa na Idara ya Elimu ya Uingereza inaonyesha kuwa, shule hiyo ndio bora zaidi nchini humo katika kuandaa mazingira ya mafanikio kwa mwanafunzi baada ya kutokuwa na kiwango kizuri kwenye shule ya msingi.
Mbali na shule ya Tawhidul Islam, zipo shule nyingine kadhaa za Kiislamu nchini Uingereza ambazo wanafunzi wake wamefanya vizuri na kuongoza kwenye taasisi za kielimu nchini humo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, kuna karibu Waislamu milioni mbili na nusu nchini Uingereza na kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Waislamu nchini humo kuna karibu wanafunzi laki nne ambao wanasoma katika shule mbalimbali. 1194144
captcha