Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumatani mjini Tehran aliponana na maelfu ya wananchi wa matabaka tofauti. Huku akitoa nasaha zake kwa matabaka yote ya wananchi wa Iran hususan vijana za kuwataka wastafidi vizuri na fursa, nafasi na uwezo mkubwa wa mwezi mtukufu wa Rajab kwa ajili ya kujijenga kimaanawi, ameutaja uchaguzi wa Rais wa Juni 14 nchini Iran kuwa ni jaribio jingine lenye fakhari kubwa kwa taifa la Iran na vile vile amebainisha malengo yanayogongana kati ya taifa la Iran na maadui wa taifa hili katika uchaguzi huo na kusisitiza kwamba: Wananchi wanapaswa kushiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika uchaguzi huo ili sambamba na kufanikisha malengo yao na kukwamisha njama za maadui, waweze pia kuchagua mtu anayestahiki zaidi, mwenye maingiliano mazuri na watu, muumini, mwanamapinduzi, "mtu wa istikama, mwenye azma thabiti na asiyetetereka" na mtu mwenye hima ya kijihadi kati ya watu watakaopitishwa na Baraza la Kulinda Katiba kwa mujibu wa misingi iliyowekwa na sheria ili mtu huyo atakayechaguliwa na wananchi na kuwashinda wagombea wengine, aweze kubeba jukumu zito la kudumisha na kupeleka mbele heshima na maendeleo ya taifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja uchaguzi wa mwezi unaokuja wa rais nchini Iran kuwa ndilo suala muhimu zaidi kwa hivi sasa nchini na huku akiashiria athari za muda mfupi na muda mrefu za jambo hilo amesema kuwa: Ingawa katika uchaguzi huo, mtu mmoja anapewa jukumu na wananchi kupitia uchaguzi la kusimamia mustakbali wa nchi na masuala makuu ya taifa kwa muda wa miaka minne lakini baadhi ya maamuzi na vitendo vizuri au vibaya vya mtu huyo vinaweza kuiathiri nchi hata kwa muda wa miaka 40 mengine na kwamba uhakika huo unaonesha ni kiasi gani uchaguzi wa Rais ulivyo na umuhimu nchini.
Aidha amebainisha umuhimu mkubwa zaidi wa uchaguzi wa Juni 14 nchini Iran na kuongeza kuwa: Ijapokuwa umebakia karibu mwezi mzima hadi kufikia wakati wa kufanyika uchaguzi huo, lakini tayari suala hilo hivi sasa limekuwa moja ya masuala muhimu sana kimataifa na kwamba maadui wa Iran na wanafikra wao wanafuatilia kwa karibu sana hata matayarisho na hatua za maandalizi tu za uchaguzi huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, madui wana malengo tofauti kabisa na malengo ya wananchi wa Iran katika uchaguzi huo na kuongeza kwamba: Wananchi wa Iran wanamtaka mtu anayestahiki zaidi kupewa jukumu hilo ambaye ataweza kuipeleka mbele nchi kwa kasi kubwa zaidi katika nyuga za kimaada na kimaanawi sambamba na kutatua matatizo yaliyopo hivi sasa kama ambavyo wanamtaka mtu wa kuweza kuwaletea maisha bora zaidi na ya ustawi zaidi na ambaye atalinda heshima na uhuru wa Iran chini ya kivuli cha hamasa, shauku na matumaini ya wananchi.
Ameongeza kuwa: Hata hivyo adui anafanya njama za kupunguza hamasa ya wananchi ya kushiriki kwenye uchaguzi huo kwani maadui wanataka mtu asiye na sifa hizo awe Rais wa Iran na kulifanya taifa hili liwe tegemezi, dhaifu, lililobaki nyuma katika nyuga tofauti na ambalo litakuwa linafuata njia ya siasa za mabeberu na watu baki.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an kabla ya jambo lolote, mabeberu walikuwa wanataka uchaguzi wenyewe usifanyike lakini kwa vile wameona kuwa hawawezi kuzuia kufanyika uchaguzi huo sasa wanafanya njama za kuwakatisha tamaa wananchi wa Iran na kuwavunja moyo ili kuufanya uchaguzi huo usiwe wa kufana na usizae matunda yanayotakiwa.
Amesema, kuwavunja moyo wananchi na kuwafanya wasishiriki kwenye uchaguzi huo ni katika ujanja na hila kubwa zinazotumiwa na adui. Ameongeza kuwa: Maadui wanataka kuzifanya fikra za walio wengi ziamini kuwa hakuna faida yoyote kushiriki katika uchaguzi huo na wala kupiga kura, hivyo kwa nini washiriki kwenye uchaguzi?
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi wa propaganda ambazo zimekuwa zikipigwa na vyombo vikubwa vya habari pamoja na mashirika ya habari ya Kizayuni katika wiki za hivi karibuni na kuongeza kuwa: Kujaribu kuonesha kuwa hali ya Iran ni ya mgogoro, kukuza kupindukia matatizo, kuwavunja moyo wananchi kuhusu uwezekano wa kutatuliwa matatizo hayo na kujaribu kuonesha kuwa mustakbali wa taifa la Iran umegubikwa na kiza totoro ni miongoni mwa makri na ghiliba zinazotumiwa na vyombo vikubwa vinavyoeneza uongo na upotofu vya maadui kwa ajili ya kutaka kuzuia uchaguzi wa Iran usifanyike kwa ufanisi mkubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an hatukatai kuwa kuna matatizo kama vile ughali wa bidhaa na ukosefu wa kazi nchini, lakini ni nchi gani duniani isiyo na matatizo? Je, kelele zote hizi zinazopigwa na wananchi wa Ulaya wanaomiminika barabarani kila siku kulalamikia jinsi matatizo yalivyozifika kooni nchi za Ulaya na jinsi wasivyoweza kuvumilia tena matatizo hayo, si mgogoro huo uliozikumba nchi hizo za Ulaya? (Hivyo hakuna nchi isiyo na matatizo katika dunia hii).
Ayatullah Udhma Khamenei amepimisha hali iliyo nayo Iran hivi sasa na nchi nyinginezo duniani na kusema kuwa: Ni nchi gani nyingine duniani iliyo na uhuru wa kitaifa, mshikamano na umoja wa kitaifa kuishinda Iran? Ni nchi gani katika dunia hii iliyo na vijana wengi kiasi chote hiki wanaoshiriki kwa hamasa ya hali juu na kupata ushindi katika medani adhimu za kielimu kuishinda Iran? Ni taifa gani lililoweza kuwa na umuhimu, adhama na taathira kama ya taifa la Iran katika matukio ya kieneo na kimataifa? Na ni taifa gani jengine ghairi ya Iran lenye watu azizi kama hawa ambalo limeweze kushinda njama zote hizi za kikhabithi za maadui na hatimaye kuweza kuvuuka kwa ufakhari mkubwa katika medani zote huku likiwa na matumaini makubwa ya mustakbali wake bora?
Baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu medani ya mapambano ya kisaisa ya taifa la Iran dhidi ya kambi ya maadui wa taifa hili amesisitiza kuwa: Wananchi wanapaswa kujua kuwa, kushiriki kwao kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika uchaguzi huo kutaiwekea kinga nchi na kutapunguza tamaa za maadui za kufanya ukhabidhi na uafiriti wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewasihi kwa kusisitiza viongozi, wanarakati wa kisaisa na watu wa majukwaani kuchukua tahadhari kubwa katika maneno na matendo yao na kuongeza kuwa: Mnapaswa kuwapa matumaini wananchi kwani mtu yeyote mwenye insafu na anayeangalia mambo kwa uhakika wake, ataona kwa uwazi jinsi taifa la Iran lilivyo na mustakbali mzuri kutokana na mambo yanavyoendelea nchini na kwa jinsi taifa la Iran lilivyo na azma na nia ya kweli katika jambo hilo.
Aidha ametoa majumuisho ya namna fulani kuhusu matokea ya mapambano kati ya taifa la Iran na maadui katika medani ya uchaguzi na kuongeza kuwa: Kulingana na welewa nilio nao kuhusu wananchi wa Iran na kwa jinsi tulivopata uzoefu wa msaada na taufiki ya Mwenyezi Mungu katika matukio ya huko nyuma, nina uhakika kuwa hivi sasa pia taifa la Iran litapata fakhari nyingine ya kuongezea kwenye fakhari zake nyingine za huko nyuma na litatoa pigo jingine kubwa kwa adui.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kiujumla vielelezo vya mtu bora zaidi na aliye na sifa bora zaidi za kuweza kuchaguliwa na wananchi kuwa Rais akisema kuwa; kabla ya kufanyika uchaguzi wa Juni 14 atatoa tena nukta zinazopaswa kuzingatiwa katika jambo hilo lakini nukta muhimu anazopenda kuashiria hapa ni kuwa, watu kabla ya kupiga kura wanapaswa wawe na ufahamu sahihi na mzuri kuhusu mtu wanayempigia kura na hilo linawezekana kwa mashauriano, kwa kutafakari na kwa kupata yakini na hujja ya kisheria kuhusu mtu anayestahiki zaidi kumchagua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia udharura wa kuchagua watu ambao hima yao ni kulinda heshima na maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa: Mambo yote tuliyofanikiwa kuyapata katika kipindi cha miongo hii mitatu, tumeyapata kwa baraka za harakati na juhudi za kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, hivyo tunapaswa kuchagua watu ambao wanalifanya suala la kufanikisha malengo hayo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ajenda yao kuu katika mazingira yoyote yale.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria wajibu wa wagombea kuwa macho katika nara na kaulimbiu zao na kukumbusha kuwa: Baadhi ya wakati wagombea wanaweza kutoa ahadi na kaulimbiu ambazo ziko nje ya uwezo wa Rais na uwezo wa nchi ili kuwavutia watu wawapigie kura, lakini wananchi nao wako macho na wanatafuta watu ambao wanatoa ahadi na kaulimbiu zilizosimama juu ya misingi ya ukweli na wanafuatilia mtu ambaye mbinu na sera zake zina uwezo wa kutatua matatizo ya wananchi na ambazo zinakubaliana na hali halisi ilivyo nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinsi watu wa kila namna walivyojitokeza kujiandikisha kuwa wagombea katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa: Baraza la Kulinda Katiba ambalo linaundwa na watu wacha Mungu, watu wema na wenye welewa mkubwa wa mambo, ndilo lililopewa jukumu hilo na sheria la kuweza kupitisha watu waliotimiza sifa za kugombea na kwamba wananchi watachagua mtu ambaye ni bora zaidi na anayestahiki zaidi kuwa Rais wao kati ya watu watakaopitishwa na Baraza la Kulinda Katiba.
Ayatullah Udhma Khamenei kwa mara nyingine amesisitizia wajibu wa kushikamana vilivyo na kikamilifu na sheria na kuongeza kuwa: Kutekeleza mambo kwa mujibu wa sheria ni kielelezo kizuri sana na ni njia bora ya kudumisha utulivu na ustawi wa taifa pamoja na kulinda umoja wa kitaifa na kwamba mtu yeyote yule hapaswi kufanya mambo kinyume cha sheria kwa hali yoyote ile.
Vile vile ameyataja matukio yaliyotokea mjini Tehran baada ya uchaguzi wa Rais wa mwaka 2009 na kulisababishia taifa hasara, yaliyotokana na kwamba baadhi ya watu walikataa kuheshimu sheria na kuongeza kuwa: Watu hao kutokana na malengo yao binafsi, au malengo yao ya kisiasa au malengo yao mengine yoyote, walitenda mambo kinyume cha sheria na matokeo yake ni kwamba mbali na kujisababishia matatizo wao wenyewe na kwa taifa na wananchi, waliwaharibia pia wananchi kufaidika vizuri na utamu wa kura za watu milioni 40 zilizopigwa kwenye uchaguzi huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kujisalimisha mbele ya sheria na kuitii ndiyo njia pekee sahihi inayotakiwa kufautwa na kuongeza kuwa: Baadhi ya wakati sheria inaweza isiwe sahihi mia kwa mia, lakini ni bora kuwa na sheria kulikoni kutokuwa kabisa na sheria.
Ameongeza kuwa: Kuna uwezekano pia kwamba mwendeshaji fulani wa sheria akafanya kosa katika sehemu fulani, na hata kama tutashindwa kurekebisha kosa hilo kwa njia za kisheria basi kuishi na sheria ya namna hiyo ni bora kulikoni kutokuwa na sheria kabisa au kutenda mambo kinyume cha sheria.
Ameongeza kwamba, kuwa na hujja ya kisheria katika suala zima la kumchagua mtu ni jambo linalodumisha utulivu wa duniani na Akhera na kuongeza kuwa: Kama kutachukuliwa uamuzi fulani kwa kutegemea sheria na uamuzi huo ukaja ukaonekana ni makosa, mchukuaji wa uamuzi huo huhesabiwa kuwa ametimiza wajibu wake na hawezi kulaumiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo kuwa, mwezi wa Rajab ni mwezi wa kujiandaa kwa ajili kuimarisha uwezo wa kimaanawi wa mtu na kuongeza kuwa: Kama mtu atapata taufiki ya kujijenga vizuri kimaanawi katika miezi ya Rajab na Shaaban na kuweza mtu huyo kuingia katika ulimwengu usio na mwisho wa umaanawi wa Mwenyezi Mungu katika hali zake zote, basi huwa amejiandalia uwanja mpana na mwafaka kabisa wa kuingia kwa njia bora mno katika ugeni usio na mipaka ambao Mwenyezi Mungu anawaalika ndani yake waja Wake wema katika mwezi uliojaa baraka wa Ramadhani.
Vile vile amekutaja kushiriki wananchi wa matabaka yote na hasa vijana katika sunna bora ya itikafu ndani ya mwezi wa Rajab kuwa kunatoa taswira nzuri sana ya kuvutia na kuongeza kuwa: Baraka, mafanikio na matunda yote haya mazuri ya Mapinduzi ya Kiislamu yamepatikana kwa msaada wa hazina hiyo kubwa ya kimaanawi na kiroho.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Sifa alizokuwa nazo Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) za kusimama kidete, uwezo wake mkubwa wa kujenga hamasa, kuanzisha kwake harakati na kuwa na nguvu za aina yake za kukabiliana na madhalimu duniani zote hizo zilitokana na machozi ya mwanachuoni huyo mkubwa mbele ya Muumba wake na jinsi Imam alivyojipinda kwa ibada na kunyenyekea kwa ikhlasi kubwa kwa Mwenyezi Mungu na jinsi Imam wetu huyo azizi alivyokuwa akikesha nyakati za usiku kunyenyekea na kumlilia Mola wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameutaja utawa katika Uislamu kuwa una maana ya kujisalimisha mtu kwa Mwenyezi Mungu katika kila kipengee cha maisha yake na amewashukuru vijana wa Iran kwa jinsi wanavyojibidiisha kuzijenga nafsi zao kiimani na kwa hisia za kimapinduzi na kuwa macho wakati wote katika medani akiongeza kuwa: Kulindwa, kuimarishwa na kutiwa nguvu moyo huyo, kutadhamini kuendelea kushuhudiwa baraka, neema na misaada ya Mwenyezi Mungu kwa taifa la Iran.
1228850