IQNA

Wabahrain waandamana kumuunga mkono Sheikh Qasim

21:22 - May 21, 2013
Habari ID: 2537043
Maandamano ya kulalamikia hatua ya askari wa usalama wa Bahrain ya kuvamia nyumba ya Sheikh Issa Ahmed bin Qassim mwanazuoni maarufu wa nchi hiyo, bado yanaendelea.
Katika kuendeleza siasa za ukandamizaji dhidi ya matakwa ya haki ya wananchi wa Bahrain, Ijumaa iliyopita makumi ya askari wa utawala wa Aali Khalifah walishambulia nyumba ya Sheikh Issa Qassim katika mji wa al Diraz magharibi mwa mji mkuu Manama na kusababisha hasara kubwa. Katika kuendelea kupinga hatua hiyo, jana wananchi wa Bahrain walijitokeza kwa wingi mabarabarani ukiwemo mji mkuu Manama, ambapo sambamba na kupiga nara za kulalamikia hatua za ukandamizaji wametaka utawala wa Aali Khalifah uache kuwanyanyasa maulamaa. Vilevile kutokana na wito uliotolewa na makundi ya maulamaa wa kidini wa kulalamikia kuvamiwa nyumba ya Sheikh Qassim, hauza za kidini za Bahrain pia zilifungwa na maulamaa pamoja na wanafunzi wa vyuo hivyo kukusanyika katika msikiti mkuu wa Imam Swadiq (A.S) katika eneo la al Diraz, kwa ajili ya kuonyesha mshikamano wao na sheikh huyo mkubwa wa madhehebu ya Kishia. Hauza za Bahrain pia zilitoa tamko lililolaani kitendo hicho na kueleza kwamba, kushambuliwa nyumba ya Sheikh Qassim ni kitendo cha kikatili kinachokusudia kuvuruga zaidi hali ya nchi hiyo na kuifanya iwe na mustakbali usioeleweka. Maulamaa maarufu wa Bahrain akiwemo Seyyid Jawad al Wada'i, Seyyid Abdallah al Gharifi, Seyyid Abdullah Hussein Sattari na Sheikh Muhammad Swaleh ar Rabi'i, pia wametoa tamko la kulaani kitendo hicho na kusema kuwa, waliotekeleza kitendo hicho cha kishenzi wanapaswa kuadhibiwa. Makundi ya kisiasa na wapinzani wa utawala wa kifalme wa Bahrain pia wamelaani kitendo hicho. Sheikh Hussein al Daihi Katibu Mkuu msaidizi wa Harakati ya al Wifaq amekemea vikali hatua hiyo na kusema kwamba, kumvunjia heshima sheikh Qassim na kushambulia nyumba yake ni sawa na kutangaza vita dhidi ya taifa la Bahrain.

Kushambuliwa nyumba ya sheikh Qassim na vikosi vya usalama vya Bahrain pia kumelaaniwa kieneo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Abbas Araqchi ameeleza kusikitishwa sana na kuvunjiwa heshima nyumba ya sheikh huyo maarufu wa Bahrain na kulaani kitendo hicho. Araqchi amesema, njia pekee ya kutatuliwa mgogoro wa Bahrain ni kutumiwa njia za kisiasa na kuzingatiwa matakwa muhimu ya wananchi, na kusisitiza kuwa, kutumiwa vurugu na vitisho pamoja na kuingia kwa mabavu katika nyumba za watu hakuendani na mantiki wala vigezo vyote vya kimaadili, dini na ubinadamu. Vilevile marjaa wakubwa wa mjini Qum akiwemo Ayatullah Nassir Makarim Shirazi na Ayatullah Nuri Hamedani wamelaani kitendo hicho, na pia maulamaa wa Lebanon. Inafaa kuashiria hapa kuwa, kwa zaidi ya miaka miwili sasa Bahrain inashuhudia maandamano ya wananchi na harakati za kimapinduzi dhidi ya utawala wa Aali Khalifa. Hii ni katika hali ambayo askari usalama wa nchi hiyo wakishirikiana na vikosi vamizi vya Saudi Arabia wanawakandamiza wananchi na kujaribu kuzima harakati hiyo, ambapo hadi sasa mamia ya watu wameuawa, kujeruhiwa na kutiwa mbaroni. Licha ya ukandamizaji huo, wananchi wanamapinduzi wa Bahrain bado wanaendelea kuandamana kudai matakwa yao, ambayo ni pamoja na kutekelezwa uadilifu katika jamii na kuwepo madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi.
1231111
captcha