Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema punde baada ya kupiga kura kwamba, maadui wa Iran wamejaribu kutumia kila njia kuwashawishi wananchi kutoshiriki uchaguzi wa rais lakini njama zao zimefeli na zitazidi kufeli kwani idadi iliyoshuhudiwa hadi sasa katika vituo vya kupigia kura ni kubwa mno. Ayatullah Khamenei amesema matokeo ya mwisho yatadhihirisha wazi mapenzi ya Wairani kwa nchi yao na imani walionayo kwa mfumo. Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa mbili asubuhi na hadi sasa foleni ndefu za wapiga kura zinaendelea kuonekana katika maelfu ya vituo hapa Tehran na nchi nzima kwa ujumla.
Duru ya 11 ya uchaguzi wa rais imewavutia wagombeaji 6 ambao ni; mwakilishi mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia Saeed Jalili, kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Mohsen Rezai, mwakilishi wa zamani wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia Sheikh Hassan Rohani, waziri wa zamani wa Mawasiliano Mohammad Gharazi, meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Ali Akbar Velayati.
Wakati huo huo mjumbe moja wa Kamati ya Utendaji ya Kituo cha Uchaguzi nchini Iran amesema kuwa, hadi Ijumaa alasiri, zaidi ya asilimia 70 ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura walikuwa tayari wameshiriki katika duru ya 11 ya uchaguzi wa rais na duru ya nne ya uchaguzi wa mabaraza ya miji na vijiji hapa nchini.
Bw. Ismail Kauthari ameongeza kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi zaidi mikoani na vijijini.
Muda wa upigaji kura umeongezewa mara kadhaa jambo ambalo linaonesha wazi kuwa asilimia ya watu walioshiriki kwenye zoezi hili muhimu itakuwa kubwa zaidi ya hiyo.
1242346