IQNA

Rais-mteule Dkt. Rohani asema Iran inapinga vita baina ya Waislamu

11:25 - July 14, 2013
Habari ID: 2560990
Rais-mteule wa Iran Hassan Rohani amesema Tehran inapinga vikali vita na mizozano baina ya Waislamu na kwamba itajaribu kila liwezekanalo kuzuia hali kama hiyo.
Akizungumza Jumamosi kwa njia ya simu na Rais Moncef Marzouki wa Tunisia, Dkt. Rohani amesema, 'Iran inapinga vita na umwagaji damu baina ya Waislamu iwe ni katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani au mwezi mwingine wowote ule.' Rais wa Tunisia alimpigia simu Dkt. Rohani kumpongeza kwa munasaba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na vile vile kwa munasaba wa kuchaguliwa kwake kuwa rais wa Iran.
Aidha rais wa Tunisia ametaka Iran isaidie katika utekelezwaji wa usitishaji mapigano nchini Syria katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Katika mazungumzo hayo, rais-mteule wa Iran amesisitiza kuwa nchi zote za Kiislamu zinapaswa kuzuia vita, makabiliano na umwagaji damu miongoni mwa Waislamu. Kuhusiana na hali nchini Misri, Rohani ameelezea matumaini yake kuwa matukio katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika yataenda sambamba na maslahi ya Wamisri.
Kwa upande wake, rais wa Tunisia amesema nchi yake haifurahishwi na mgogoro ulioko Misri. Ameongeza kuwa Tunis itajitahidi kushirikiana na wengine kurejesha utulivu Misri na katika nchi zote za Kiislamu zinazokumbwa na mizozo.

Dkt. Rohani alichaguliwa kuwa Rais wa Iran katika uchaguzi wa Juni 14 uliohudhuriwa na asilimia 72 ya wapiga kura ambapo alipata asilimia 50.7 ya kura zote milioni 36 na laki saba zilizopigwa.

Rohani anatazamiwa kuapishwa katika wiki ya kwanza ya mwezi ujao wa Agosti na kuchukua nafasi ya Rais anayeondoka Mahmoud Ahmadinejad.

1257318
captcha