Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran Ayatullah Ahmad Janati, amesema kuwa, hali ya mambo ya nchini Misri na kuendelea mapigano na mauaji nchini humo, ni mambo yanyotia wasiwasi mkubwa.
Ayatullah Ahmad Janati amesema kuwa, miongoni na mambo yaliyopelekea kushuhudiwa matatizo na mgogoro wa hivi sasa nchini humo, ni misimamo isiyo sahihi iliyochukuliwa na Rais Muhammad Mursi kuhusiana na utawala haramu wa Kizayuni. Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran ameongeza kuwa, hatua ya serikali ya Mursi ya kufunga kivuko cha Rafah kilichoko katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na Misri, kukumbatia mkataba wa Camp David, kuendelea kutuma mafuta kwa utawala wa Kizayuni na kuendeleza mahusiano ya kirafiki na utawala huo, ilikuwa ni kwenda kinyume na matakwa ya wananchi wa Misri, suala lililoibua hasira kali za wananchi hao. Akiashiria kuwa wananchi wa Misri, wanataka uhuru na kujitegemea, amewataka raia wa nchi hiyo, kulinda umoja wao na kuangalia mambo yanayowaunganisha kuhusu nchi yao ili waweze kufikia makubaliano na kukomesha haraka umwagikaji damu kwani jambo hilo halina faida kwao ghairi ya kuwaletea faida maadui. Aidha khatibu wa Sala ya Ijumaa ya hapa mjini Tehran, ameashiria mauaji ya kijana mwenye asili ya Kiafrika huko nchini Marekani, mauaji yaliyofanywa na Mmarekani mmoja mzungu na hatua ya mahakama moja ya nchi hiyo kumuondolea hatia mzungu huyo muuaji na kusema, hatua hiyo inabainisha ni namna gani Marekani inavyokanyaga waziwazi haki za binaadamu nchini humo.
1259865