IQNA

Imam Khamenei asema Wamarekani hawaaminiki

22:31 - July 22, 2013
Habari ID: 2565437
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Wamarekani hawaaminiki, wasiotumia mantiki na sio wakweli wa kufanya nao miamala.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumapili jioni alipoonana na viongozi na wafanyakazi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, mchakato wa kukabidhi majukumu ya utekelezaji (Serikali) ni fursa yenye baraka nyingi katika kuendelea na utekelezaji wa fikra za Imam Khomeini (quddisa sirruh) kwenye masuala tofauti ya nchi.
Vile vile amebainisha matukio ya kihistoria na ya hivi sasa ya nchini Iran na kusisitiza kwamba: Suala la uchumi na kuendelea kushuhudiwa maendeleo ya kielimu ni katika mambo ambayo inabidi yawe ni vipaumbele vikuu kwa viongozi wote nchini Iran.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa uhai wa kuupata mwezi mwingine mtukufu wa Ramadhani na kunufaika na baraka za mwezi huu na kuongeza kuwa: Moja ya majukumu ya mwanadamu ni kwamba kila baada ya kupata nusra na ushindi fulani kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, aongeze unyenyekevu na utiifu wake kwa Mwenyezi Mungu.
Ameashiria ushindi na nusra ya mfululizo linayopata taifa la Iran kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Ushindi na nusra ya karibuni kabisa ya Mwenyezi Mungu liliyoipata taifa la Iran ni ushindi mkubwa wa kuweza kuunda hamasa kubwa ya kisiasa katika uchaguzi uliopita wa Rais ambapo athari za hamasa hiyo adhimu zitaonekana pole pole katika sekta mbali mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kukaribiana nyakati za harakati kubwa ya kisiasa ya taifa la Iran na mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni taufiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Mwezi wa Ramadhani ambao ni mwezi wa rehema na maghufira ya Mwenyezi Mungu na ni mwezi wa toba na kurejea kwa Mwenyezi Mungu ukiwa na Baraka nyingi sana na dua na amali bora za kila namna, ni uwanja mzuri wa kuweza mwanadamu kunyenyekea zaidi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba watu wote wanapaswa kuitumia vizuri fursa hii kubwa na ya kipekee.
Vile vile ameashiria wajibu wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu wakati wote iwe ni wakati wa dhiki au wakati wa raha na stararehe na kusema kuwa, kufanya hivyo kunatoa dhamana ya kushuhudiwa harakati ya kujikamilisha mwanadamu na kusisitiza kuwa: Kumkumbuka na kumzingatia huko Mwenyezi Mungu kunapaswa kuwe sababu ya kutenda amali njema na kama itafanyika hivyo basi kudorora, kuzorota, kukosa matumaini kukata tamaa na kurudi nyuma yatakuwa ni mambo yasiyo na nafasi kabisa kwa watu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, miongoni mwa mambo ya lazima ya kuweza kufanikisha amali hiyo ni subira na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kusisitiza kwamba: Subira maana yake ni kusimama kidete, ni muqawama na kutosahau malengo; na kutawakali maana yake ni watu kutekeleza inavyopasa majukumu yao na kuchapa kazi kwa nguvu zao zote na halafu kumwachia Mwenyezi Mungu matokeo ya kazi zao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiairia pia nafasi ya subra na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu katika amali za watu binafsi na vile vile katika masuala yanayohusiana na uendeshaji wa nchi na kusema kuwa, kuna mambo mawili makuu yenye nafasi kubwa katika kustafidi na mambo hayo mawili muhimu. Amesema: Jambo la kwanza ni kuchagua upande ulio sawa na kuulinda upande huo sahihi.
Amekumbusha pia kuwa: Iwapo njia za kufuatwa hazitachaguliwa kwa njia sahihi basi hata kama juhudi zitafanyika maradufu hazitaweza kutufikisha kwenye malengo yetu bali zitatuweka mbali na malengo yetu hayo matukufu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu njia sahihi za kufuatwa katika kuongoza nchi na kukumbushia matamshi yake aliyoyatoa katika maadhimisho ya kukumbuka siku aliyofariki dunia Imam Khomeni (quddisa sirruh) na kuongeza kuwa: Siku hiyo nilisisitiza kuwa njia sahihi ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya nchi iko wazi katika nyuga zote kutokana na busara kubwa alizotuwekea Imam (Khomeini - quddisa sirruh) na hakuna haja ya kufanya utafiti mpya wa kutafuta njia za kufuata.
Amemtaja Imam kuwa ni mwanachuoni, mtu mwenye hekima na fakihi aliyebobea ambaye alikuwa na busara kubwa na mweledi wa mambo na kuongeza kuwa: Fikra za Imam zinazopatikana katika hotuba zake, katika maandishi na athari zake ukiwemo wasia wa mwanachuo huyo mkubwa, ziko wazi kabisa na ni muongozo muhimu wa kufuatwa na watu wenye vipaji, viongozi, watu wenye ushawishi na matabaka mbali mbali ya wananchi ingawa tab'an baadhi ya wakati kunatolewa tafsiri isiyo sahihi kuhusu fikra na mitazamo ya Imam, jambo ambalo ni baya na la hatari sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Njia sahihi za kufuatwa zilizobainishwa na Imam (Khomeini - quddisa sirruh) zinapaswa kupewa nafasi kubwa na ya kimsingi katika siasa kuu na ndogo ndogo za uendeshaji wa nchi.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia mambo yenye nafasi katika subira na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu katika kuongoza nchi na kutumia mbinu na suhula zote pamoja na kuainisha vipaumbele katika mambo mbali mbali na baada ya hapo amezungumzia kiujumla masuala mbali mbali yaliyopo hivi sasa nchini Iran.
Mwanzoni mwa kuzungumzia suala hilo, Ayatullah Udhma Khamenei amevitaja vipindi mbali mbali vya kukabidhi majukumu ya serikali tofauti nchini kuwa ni vipindi na nyakati nzuri na zilizojaa baraka na kuongeza kuwa: Kuingia watu wapya, fikra mpya, ubunifu na mirengo mipya katika medani ya kukabidhiana madaraka ni sikukuu na ni fursa kubwa ambayo inabadi itumike vizuri sana.
Ameongeza kuwa: Alhamdulillah katika vipindi vyote vya kukabidhiana madaraka, ukitoa mwaka 2009 ambapo baadhi ya watu walifanya kosa kubwa na kuifikisha pabaya nchi, siku zote vipindi hivyo vimekuwa vizuri na vinavyopita kwa furaha na bashasha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Majimui, watu au kundi linaloigia katika medani likiwa na fikra na ubunifu mpya linapaswa kustafidi pia na kazi zilizofanyika hadi hivi sasa nchini ili kwa njia hiyo lizidi kuiimarisha nchi na kuipandisha juu kimaendeleo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia kazi nyingi na kubwa zilizofanywa na serikali ya hivi sasa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, majimui yoyote ile ya watu inapaswa kuwa na mtazamo chanya na mzuri kuhusu majimui ya kabla yake na ni vyema vilioje ikiwa serikali ya baadaye nayo itachapa kazi kwa kiwango hiki hiki au kwa kiwango kikubwa zaidi cha kazi na jitihada za kuliletea taifa maendeleo.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja masuala 7 na kuyajadili kiujumla masuala hayo katika hotuba yake hiyo.
Miongoni mwa mambo yaliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu hiyo ya hotuba yake ni pamoja na nafasi bora kabisa ya kijiografia iliyo nayo Iran, historia yake iliyojaa fakhari pamoja na ustaarabu wake mkongwe uliokita mizizi, utajiri wake mkubwa wa maliasili na kuwa kwake na watu wenye vipaji vikubwa. Mambo hayo matatu ndiyo aliyoanza kuyaashiria Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenye sehemu hiyo ya hotuba yake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria suala la nne kwa kusema: Katika kipindi cha karne mbili au tatu zilizopita, Iran imepata hasara kubwa sana kutokana na tawala kandamizi na za kidikteta na ushawishi na mashambulizi ya kiutamaduni na kisiasa ya wageni na inabidi kila moja ya mambo hayo lipewe uzito wake unaotakiwa katika kulichanganua na kulichunguza.
Vile vile ametaja mwamko wa kitaifa na wa watu wote katika nyakati tatu tofauti, wakati wa utawala wa katiba, wakati wa kufanywa mafuta ya Iran kuwa ni mali ya taifa na wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba ni masuala mengine muhimu yaliyotokea nchini Iran na kuongeza kuwa: Ingawa harakati ya wananchi wa Iran ya kusimama kidete kupigania haki yao katika kipindi cha utawala wa katiba na mwamko wa taifa ilivunjwa, lakini ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran yamekuwa ni majibu sahihi kabisa ya kufidia hasara ilizoingizwa Iran kutokana na uvamizi na mashambulizi ya wageni.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja harakati ya taifa la Iran iliyopata mafanikio na ushindi katika nyuga tofauti za kisiasa, kiuchumi, kielimu na kiutamaduni kuwa ni suala la muhimu lililotokea nchini Iran ambalo linapaswa kuzingatiwa katika mtazamo na fikra jumla na kuu ya nchi.
Ameongeza kuwa: Maendeleo ya kustaajabisha yaliyopigwa na Iran katika upande wa kielimu na jinsi mtu yeyote asivyoweza kukanusha jinsi Iran ilivyo na taathira katika masuala muhimu ya kieneo na tab'an masuala ya kimataifa pia; maendeleo ya ajabu katika upande wa ujenzi wa nchi na kubadilika kwa daraja 180 masuala ya utamaduni ikilinganishwa na kipindi cha utawala wa taghuti nchini Iran, ni miongoni mwa ishara za kuweko harakati ya ushindi katika kipindi hiki cha miaka 30 iliyopita nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja demokrasia ya kidini na demokrasia salama kuwa ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kisiasa yaliyopatikana ndani ya Iran na kuongeza kuwa: Mchakato wa kukabidhiana madaraka kwa njia salama na ya kiukweli iwe ni kutoka Serikali moja hadi nyingine au kutoka Bunge moja hadi jingine tena bila ya kutumia ujanja na wala hila za kisiasa kama ilivyozoeleka katika nchi za Magharibi ni modeli mpya na yenye thamani kubwa ambayo taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya imeibuni na kuiarifisha kwa walimwengu.
Amma katika upande wa maendeleo ya ndani ya Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mustakbali uliojaa matumaini unaowasubiri vijana wa Iran na kuongeza kuhusu maudhui hiyo kwamba: Suala la kujizuia kuzaa watoto ni hatari kubwa hasa baada ya wataalamu na wasomi wa masuala hayo kuthibitisha kuwa Iran inaelekea kukumbwa na tatizo la kuwa na watu vizee na matatizo mengine mengi, hivyo inabidi suala hilo lizuiwe.
Aidha ametoa mwito kwa wabunge kulizingatia sana suala hilo na kuutia nguvu mpango unaojadiliwa bungeni hivi sasa kuhusu kuzuia jambo hilo.
Suala la mwisho ambalo Ayatullah Udhma Khamenei amelianasiri katika mtazamo wake jumla kuhusu nchi na taifa la Iran ni kadhia ya uadui mkubwa na wa muda mrefu wa maadui na watu wenye chuki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema: Fikra finyu na ubeberu wa baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi na baadhi ya viongozi dhaifu wa serikali za eneo la Mashariki ya Kati kuhusiana na taifa la Iran wameanzisha kambi kubwa ya kukabiliana na taifa hili kwa namna ambayo hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kushuhudia kambi kubwa kama hiyo dhidi yake.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, masuala saba aliyoyataja ni vielelezo kuhusu njia ya mustakbali na kusisitiza kuwa: Mambo hayo saba yanaonyesha kuwa kwa hakika muongo huu wa Mapinduzi ya Kiislamu unaweza kugeuka kuwa muongo wa maendeleo na uadilifu na katika suala hilo tunaweza kusema kuwa ubunifu na uchapaji kazi wa viongozi wakuu wa sekta mbali mbali nchini kuwa ni fursa na neema muhimu ya Mwenyezi Mungu kwa taifa la Iran.
Akifanya majumuisho ya namna fulani kuhusu masuala aliyozungumzia katika hotuba yake hiyo amesema: Inabidi iundwe na iimarishwe zaidi nguvu kubwa ya ndani na ya kitaifa kwa kutegemea subira, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kusimama kidete mbele ya kambi ya maadui ili liweze taifa la Iran kuendelea na kupata maendeleo na liweze kuendelea na harakati yake ya kufanikilisha malengo makuu matukufu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi pia kuhusu mambo yanayoweza kujenga nguvu ya ndani na ya kitaifa kuwa ni pamoja na kuwa na imani ya kweli, azma na nia thabiti ya wananchi na viongozi nchini na kutotetereka katika kukabiliana na matatizo na uadui wa maadui na kuongeza kuwa: Viongozi nchini hawapaswi kutetereka hata kidogo mbele ya hamaki za maadui na vizuizi vinavyowekwa na maadui hao katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kipropaganda.
Amma kuhusiana na mambo yanayopaswa kupewa vipaumbele hivi sasa nchini Iran, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Viongozi wakuu nchini Iran, watungaji wa sera na viongozi wengine wote nchini wanapaswa kuelekeza nguvu zao na mazingatio yao zaidi kwenye vipaumbele viwili vikuu yaani suala la uchumi na suala la maendeleo ya kielimu.
Amesema: Hamasa ya kiuchumi ni sehemu moja ya kaulimbiu ya mwaka huu nchini Iran na ni matumaini yetu kuwa kama ilivyotokezea kwa hamasa ya kisiasa iliyofanikishwa vizuri sana, hamasa ya kiuchumi nayo itaweza kufanikishwa inavyotakiwa kwa hima ya viongozi nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an hamasa ya kiuchumi si kazi ya muda mfupi, lakini pamoja na hayo inabidi kazi hiyo ianze.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia kipaumbele cha pili yaani maendeleo ya kielimu na kuongeza kuwa: Kasi ya maendeleo ya kielimu nchini Iran imekuwa nzuri sana katika kipindi hiki cha miaka 10 iliyopita na haipaswi kasi hiyo kuachiwa ipungue bali inabidi kasi hiyo iendelee kwa ajili ya kufikia kwenye daraja inayotakiwa na kufikia kwenye mistari ya mbele ya elimu duniani.
Maudhui nyingine iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake ni suala la muamala na nchi nyingine duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Sisi siku zote tumekuwa na tutaendelea kuwa na msimamo wa kupenda kuwa na uhusiano mzuri na nchi nyingine duniani lakini jambo lililo muhimu katika suala hilo ni kuutambua vizuri upande wa pili na kuelewa malengo na hila zake kwani kama upande wa pili hatutaujua vizuri basi tutajikwaa.
Amesisitiza kuwa: Katika kuamiliana na nchi nyingine duniani hatupaswi kusahau vitendo vya kiadui vya maadui wetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matamsi ya hivi karibuni ya viongozi wa Marekani ya kudai kuwa wanataka kufanya mazungumzo na Iran na kusema: Hata mwanzoni mwa mwaka huu pia nilisema kuwa mimi sina imani na wala sina matumaini na mazungumzo na Marekani ingawa pamoja na hayo hata katika miaka ya huko nyuma pia mimi sikuzuia kufanyika mazungumzo ya namna hiyo kama yale yaliyofanyika katika baadhi ya masuala kama vile kwenye suala la Iraq.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Wamarekani si watu wa kuwaamini na si watu wanaotumia mantiki na si wakweli katika miamala yao.
Amesema, misimamo iliyochukuliwa na Marekani kuhusiana na Iran katika miezi hii kadhaa iliyopita ni uthibitisho mwingine wa udharura wa kutokuwa na imani na Wamarekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Kipaji cha mtu kitaonekana wakati mtu huyo ataweza kuendelea na njia yake katika kuaminiliana na nchi nyingine duniani bila ya upande wa pili kuwa na nguvu za kumzuia kwani itakuwa ni hasara kama kuamiliana huko na nchi nyingine duniani kutalipelekea taifa lirudi nyuma katika njia na harakati yake.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa masuala ya eneo la Mashariki ya Kati ni muhimu na kuongeza kuwa: Viongozi nchini Iran wanapaswa kuyazingatia sana masuala hayo.
Kabla ya hotuba hiyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti ndefu kuhusu kazi zilizofanywa na serikali katika kipindi cha miaka 8 iliyopita kwenye masuala tofauti. Ripoti hiyo ya Rais Ahmadinejad ilikuwa imegawanywa kwenye maswali 21 na majibu yake kuhusiana na kazi zilizofanywa na serikali zake kwenye miaka 8 iliyopita na kulinganisha kazi hizo na zile zilizofanyika katika serikali za kabla ya hapo. Tab'an Dk Ahmadinejad amesema kuwa, kupimisha na kulinganisha kazi zilizofanywa na serikali zake mbili kwa upande mmoja na serikali za kabla yake za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wa pili hakuna maana ya kukanusha kazi nzuri na muhimu zilizofanywa na serikali hizo zilizopita.
1261641
captcha