IQNA

Sayyid Hassan Nasrullah

Hizbullah inaungwa mkono na wananchi

14:42 - July 25, 2013
Habari ID: 2566804
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa suala muhimu kwa harakati hiyo ni kwamba inaungwa mkono na wananchi wa Lebanon, mataifa ya Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu.
Sayyid Hassan Nasrullah ambaye alikuwa akijibu hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiweka Hizbullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi, alisema Jumatano jioni katika karamu ya futari iliyotayarishwa na Hibzullah mjini Beirut kwamba, wanamapambano wa Hizbullah wamebadili kanuni za mapigano, wakabatilisha mipango ya adui na kukomboa mateka na ardhi za Lebanon zilizokuwa katika makucha ya Wazayuni na wataendelea kuwa mwiba katika jicho za Israel.

Sayyid Nasrullah amesema Hizbullah haikushangazwa na hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiweka katika orodha yake ya makundi ya kigaidi, kwani uamuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, na kwamba jambo la kushangaza ni kuchelewa uamuzi huo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema Umoja wa Ulaya (EU) unatumikia maslahi ya Israel na kwamba, umoja huo umetwishwa maamuzi hayo kwa sababu yanapingana na thamani za nchi za Ulaya.

Amesema wale wanaodhani kwamba Hizbullah ambayo ilitoa kipigo kikali kwa wavamizi wa Kizayuni hususan katika vita vya siku 33 hapo mwaka 2006 itasalimu amri mbele ya uamuzi huo usio na thamani yoyote, ama wanaota au ni majahili.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza tena kuwa, harakati hiyo ya mapambano itaendelea kuwepo na itashinda kwa uwezo wake Allah.
1263618
captcha