IQNA

Imam Khamenei apongeza demokrasia ya Kiislamu Iran

21:05 - August 04, 2013
Habari ID: 2571070
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ukabidhianaji madaraka ya urais kwa njia ya amani ni natija ya mfumo wa demokrasia ya Kiislamu nchini Iran. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo Jumamosi alasiri mjini Tehran katika hafla ya kumuidhinisha Dakta Hassan Rohani, kuwa rais wa saba wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza katika hafla hiyo Kiongozi Muadhamu alimnasihi rais na serikali mpya kufanya juhudi zisizo na kikomo na kujiepusha na hamaki katika kazi. Kiongozi Muadhamu aidha aliidhinisha nadharia ya rais mpya wa Iran kuhusu kutumia hekima katika uhusiano wa kimataifa na masuala ya kisiasa. Alisema kutokana na kuwa Iran ina maadui wasiotumia akili na mantiki, serikali ya Iran ina wadhifa wa kufanya kazi kwa hekima kwa kuzingatia malengo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullahil Udhma Khamenei pia alimshukuru Mahmoud Ahmadinejad rais wa zamani na serikali yake kwa huduma na kazi zake muhimu. Kiongozi Muadhamu aliashiria ukosefu wa utawala wa wananchi nchini Iran katika zama za utawala wa udikteta tegemezi wa Kipahlavi. Alisema kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kukita mizizi demokrasia ya Kiislamu nchini, sasa wananchi wana nafasi katika masuala yote muhimu na usimamizi wa kisiasa.Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenye mfumo wa utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi, wananchi wana nafasi na sauti katika masuala yote muhimu.

Kiongozi Muadhamu pia aliashiria matatzio ya kiuchumu na kisiasa katika Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na machafuko katika baadhi ya nchi za eneo. Alisema kuwepo utawala ghasibu, dhalimu na wenye kutenda jinai wa Kizayuni katika miaka 65 iliyopita ni kati ya matatizo ambayo yanatokana na uungaji mkono wa madola ya kibeberu. Alisema pamoja na hayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea na msimamo wake ulio wazi ili kufikia maendeleo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria pia mahudhurio makubwa ya wananchi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kubainisha kuwa siku ya Ijumaa wananchi wa Iran waliwadhihirishia walimwengu jinsi walivyosimama imara na kutangaza msimamo wao kuhusiana na Quds na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kiongozi Muadhamu ameashiria pia vikwazo vya maadui dhidi ya taifa la Iran na kueleza kwamba katika vipindi vyote vya kukabiliana na vikwazo viongozi na wananchi wa Iran wamepata tajriba na uzoefu mzuri na wenye thamani.
Aidha Ayatullah Khamenei aliashiria uhasama wa maadui wakiongozwa na Marekani dhidi ya Iran. Alisema uhasama huo umewaletea wananchi matatizo lakini kwamba hali hiyo imewapa uzoefu mkubwa wakuu na wananchi wa Iran.

Wakati huo huo Rais Hassan Rohani wa Iran amesema kuna haja ya azma ya kitaifa ya kujiepusha na misimamo ya kufurutu mipaka katika utungaji sera na usimamizi sambamba na kuzingatia utawala wa sheria.

Akizungumza katika sherehe za kuidhinishwa kwake Jumamosi, Dkt. Rohani alisema idadi kubwa ya wapiga kura katika uchaguzi walisisitiza kuhusu misimamo ya wastani. Aliongeza kuwa msimamo wa wastani ni sifa ya utamaduni wa Kiislamu-Kiirani. Rohani amesema mitazamo ya wastani haimaanishi kutoka kwenye misingi ya mapinduzi wala kupinga mageuzi.

Baada ya Kiongozi Muadhamu kuidhinisha kuchaguliwa kwake, Rohani ataapishwa leo na kuchukua nafasi ya Mahmoud Ahmadinejad ambaye mihula yake miwili ilimalizika rasmi jana. Viongozi wa nchi kadhaa wanatazamiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rohani zitakazofanyika katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani bunge la Iran.
1267702
captcha