IQNA

Rohani: Iran iko tayari kwa mazungumzo ya nyuklia

13:08 - August 07, 2013
Habari ID: 2572656
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Dkt. Hassan Rohani leo amesema Iran iko tayari kwa ajili ya mazungumzo ya 'dhati' ya nyuklia pasina kupoteza wakati.
Akizungumza katika kikao chake cha kwanza na waandishi wa habari hapa Tehran, Rohani ameongeza kuwa, mradi wa amani wa nyuklia wa Iran ni kadhia ya kitaifa na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitafumbia jicho haki hii ya watu wa Iran. Ameongeza kuwa Iran italinda haki yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Rohani amesema taarifa za hivi karibuni za Ikulu ya White House ni kielelezo cha wazi kuwa wakuu wa Marekani hawakufahamu ujumbe wa watu wa Iran katika uchaguzi uliopita. Amesema kile ambacho Iran itaangalia kuhusu Marekani ni vitendo na si maneno na kwamba Marekani inapaswa kuonesha nia njema na kuiheshimu Iran kabla ya njia ya mazungumzo kufunguliwa.

Aidha Rais wa Iran amesema vikwazo vya Wamagharibi dhidi ya Iran havitafika popote. Amesema katika kuondoa wasiwasi uliopo baina ya Iran na nchi za Magharibi kuna uwezekano wa kufikia mwafaka ambao utakuwa kwa maslahi ya pande zote. Dkt. Rohani amesisitiza juu ya azma ya taifa la Iran katika kuamiliana kwa heshima na dunia kwa msingi wa maslahi ya taifa. Ameongeza kuwa kuimarisha uhusiano na nchi jirani na kuleta utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati ni jambo ambalo litapewa umuhimu na serikali yake.
1269518
captcha