IQNA

Imam Khamenei: Marekani itapata pigo Syria

21:39 - August 28, 2013
Habari ID: 2581955
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, uingiliaji wa madola ya kieneo kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za kigeni dhidi ya nchi moja hautakuwa na natija yoyote ghairi ya kuwasha moto na kuzidisha chuki ya wananchi wa mataifa mbalimbali dhidi ya wavamizi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo katika kikao cha kwanza na serikali ya awamu ya 11 ya Iran huku akiashiria hali tete na mgogoro wa eneo la Mashariki ya Kati. Amesema, kuwasha moto katika eneo hili kutakuwa na matokeo yasiyojulikana. Amezungumzia mgogoro wa Syria, vitisho na uvamizi tarajiwa wa Marekani dhidi ya nchi hiyo kuwa ni hali ya kushangaza na kusisitiza kuwa, ikiwa hatua kama hiyo itachukuliwa, basi bila shaka Wamarekani watapata pigo kama vile walivyodhurika katika uvamizi wao huko Iraq na Afghanistan.

Vilevile ameashiria kadhia ya Misri na kusema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, haina nia ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, kama ambavyo pia haitanyamazia kimya mauaji dhidi ya wananchi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameliusia taifa la Misri kwa kusema kuwa, Wamisri wanatakiwa kujiepusha na vita vya ndani na kwamba, vita vya ndani katika nchi hiyo, vitazusha hali mbaya katika ulimwengu wa Kiislamu na eneo zima la kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati. Amesisitizia udharura wa kurejea kwenye demokrasia na kuheshimu chaguo la wananchi na kuongeza kuwa, baada ya kutawaliwa kwa miaka mingi na utawala wa kidikteta, wananchi wa Misri walifanikiwa kufanya uchaguzi halali kwa baraka za Mwamko wa Kiislamu katika nchi hiyo, hivyo ni suala la ajabu kuona demokrasia hiyo ikisimama ghafla.

Kwa upande mwingine Ayatullah Khamenei amesifu ushirikiano uliopo kati ya serikali na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge kwa ajili ya kuanza haraka utendaji kazi wa serikali.
1279701
captcha