Ayatullah Muhsin Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amewataka maulamaa wa nchi za Kiislamu kufanya juhudi za kuyatangaza mafundisho ya Uislamu kwa watu.
Ayatullah Araki ametoa wito huo Jumamosi katika kongamano la kimataifa la Umoja wa Kimataifa wa Wanawake wa Kiislamu lililofanyika hapa mjini Tehran. Akiashiria umuhimu wa umoja na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini (MA), Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amewahutubu maulamaa wa nchi za Kiislamu wakiwemo wa Saudi Arabia, Misri, Pakistan na nchi nyenginezo kwa kusema:”Fanyeni juhudi za kuwakumbusha watu mafundisho ya Uislamu; na akahoji kwa kusema, kwa nini baadhi ya watu wanachochea hitilafu katika jamii za Kiislamu?” Ayatullah Araki ameongeza kwa kuhoji tena, kwamba kwa nini wakati adui alipotishia utambulisho wa Uislamu huko Palestina hakuna mtu aliyetoa fatwa ya Jihadi, lakini leo watu wanalitumia jina la Jihadi kueneza hitilafu, kumwaga damu na kufanya mauaji katika nchi za Kiislamu? Ayatullah Araki aidha ameeleza matumaini yake kuwa Umoja wa Kimataifa wa Wanawake wa Kiislamu utaweza kuyatangaza na kuyaeneza ulimwenguni mafundisho ya Bibi Fatimatuz Zahra (AS) ambayo ndiyo mafundisho ya Bwana Mtume SAW. Kongamano la siku moja la Umoja wa Kimataifa wa Wanawake wa Kiislamu lililofanyika leo hapa mjini Tehran limehudhuriwa na shakhsia 120 wanawake wakiwemo wasomi na wanafikra mbalimbali wa Ulimwengu wa Kiislamu.
1283571