IQNA

Vikosi vya Bahrain vyawahujujumu wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani

16:46 - March 17, 2015
Habari ID: 3001292
Askari wa Bahrain wamewashambulia wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani kwa mnasaba wa kumbukumbu ya uingiliaji wa kijeshi wa Saudi Arabia nchini Bahrain, wananchi wa Bahrain wamejitokeza mitaani kulalamika na kupinga kuwepo vikosi vamizi vya Saudi Arabia katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Katika kukabiliana na wananchi wa Bahrain waliokuwa wakiandamana kwa amani, wanajeshi wa utawala Aal Khalifa wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.  Ikumbukwe kuwa Mnamo tarehe 14 Machi mwaka 2011, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Kuwait zilituma wanajeshi wao nchini Bahrain ili kuusaidia utawala wa kiimla wa Aal Khalifa kuwakandamiza wananchi wanamapinduzi wanaotaka mabadiliko nchini humo.  Katika maandamano yao, Wabahrain wamelaani kuwepo vikosi vya Saudia na Imarati nchini humo huku wakitangaza mfungamano wao na Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Chama cha upinzani cha Al Wefaq. Sheikh Salman alikamatwa na kufungwa katika jela za kuogofya za utawala wa Aal Khalifa. Waandamanaji wametaka kuachiliwa huru Sheikh Salman na wafungwa wote wa kisiasa nchini humo. Aidha wameutaka utawala kusitisha ukiukwaji wa haki za binadamu. Abdulhamid Dashti Mkuu wa Kamatiya Kiarabu ya Haki za Binadamu anasema: “Kukamatwa Sheikh Ali Salman na shakhsia wengine wapinzani ni kosa la wazi la utawala wa Bahrain na wafunwa wote wa kisiasa wanapaswa kuachiliwa huru sambamba na kuanza mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kuleta mfumo wa utawala wa wananchi waliowengi.”

Kwa upande wake Ali Sarai Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kupambana na Ugaidi na Misimamo Mikali ya Kidini ameandaa maandamano mbele ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa kulalamikia kukamatwa na kufungwa jela Sheikh Ali Salman.  Mfungwa mwingine maarufu wa kisiasa Bahrain ni Nabil Rajab ambaye kesi yake imeakhirishwa hadi mwezi Aprili.

Hivi sasa kuna maelfu ya wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain na idadi yao imekuwa ikiongezeka kila siku iendayo kwa Mungu. Kwa hakika ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa umeigeuza Bahrain na kuifanya kuwa gereza kubwa. Fauka ya hayo, wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wanaishi katika mazingira mabaya mno huku wakiandamwa na mateso ya kila aina. Malalamiko ya amani ya wananchi wa Bahrain yalianza Februari 14 mwaka 2011 na hadi sasa mashambulio ya vikosi vya utawala huo wa kifamilia vikishirikiana na vile vya Saudia dhidi ya raia yamepelekea mamia ya raia wasio na hatia kuuawa na kujeruhiwa.

Bahrain imepata kiburi cha kukiuka haki za binaadamu na kuwakandamiza kinyama wananchi kutokana na uungaji mkono mkubwa kutoka kwa madola ya Magharibi hasa Uingereza na Marekani. Mtawala wa Bahrain ni kibaraka mkubwa wa Marekani na ameigeuza nchi yake kuwa kituo kikubwa cha jeshi la wanamaji la Marekani.../mh

3000018

captcha