IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Udharura wa kuzuia upotoshaji shakhsia ya Imam Khomeini MA

22:55 - June 04, 2015
Habari ID: 3310916
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mafundisho ya Imam Khomeni MA ndio ramani ya njia ya taifa lililojaa matumaini la Iran na kwamba kuna udharura wa kukabiliana na upotoshaji shakhsia ya Imam.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo alipohutubia halaiki kubwa ya wananchi watiifu wa Iran katika Haram Takatifu ya Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini MA, kwa mnasaba wa mwaka wa 26 tokea arejee kwa Mola wake. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu alisema njia pekee ya kukabiliana na wenye kupotosha shakhsia adhimu ya Imam ni kuangazia upya misingi ya mafundisho yake. Kiongozi Muadhamu katika kubainisha maudhui asili katika hotuba yake yaani, 'Kupotoshwa Shakhsia ya Imam' ameongeza kuwa, kinyume na baadhi ambao wanajaribu kuifanya shakhsia ya Imam iwe ya zama alizokuwa hai tu, Imam alikuwa dhihirisho la harakati adhimu na ya kihistoria katika taifa la Iran. Amesema kuna haja ya kuwa macho ili kutopotosha mafundisho ya Imam Khomeini. Ayatullah Khamenei amesema mafundisho ya 'kifikra, kisiasa na kijamii' ya Imam Khomeini yanapaswa kuwa 'Ramani ya Njia ya Taifa la Iran' ili kuweza kufikia malengo makubwa kama vile uadilifu, ustawi, na uwezo wa kitaifa. Amesema pasina kufahamu mafundisho 'sahihi na yasiyokuwa yamepotoshwa ya Imam' haitawezekana kuendelea na ramani hiyo ya njia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa madola ya kiistikbari na madola makubwa ya kibeberu yangali yanaitazama Iran kwa jicho la tamaa na wanaiona nchi hii kama nchi kubwa, tajiri na muhimu katika eneo. Ameongeza kuwa: "Madola haya makubwa yataacha tamaa na ulafi wao wakati taifa la Iran litakapostawi na kupata uwezo mkubwa kiasi cha kupoteza matumaini katika njama zao.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria baadhi ya matukio katika eneo katika miaka ya hivi karibuni na namna baadhi ya mirengo ilivyoiamini Marekani na kisha kupata pigo. Ameongeza kuwa: "Imam Khomeini (MA), katika fremu ya msingi wa fikra zake, alichukua msimamo imara wa kukabiliana na Marekani na taasisi zake za kisiasa na kiusalama na wakati huo huo aliunga mkono kikamilifu mataifa yaliyodhulumiwa hasa watu wa Palestina.” Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa tunaweza kuchambua hali ya sasa ya eneo na dunia katika fremu ya mantiki ya Imam Khomeini (MA). Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo inapinga ukatili na udhalimu wa kundi la Daesh au ISII huko Iraq na Syria kama ambavyo pia inapinga sera za kidhalimu za Polisi ya Marekani ndani ya nchi hiyo na inatazama mienendo ya pande hizo mbili, yaani Daesh na polisi ya Marekani kuwa ni kitu kimoja. Ayatullah Khamenei ameendelea kusema kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vikali mzingiro dhidi ya Wapalestina wanaodhulumiwa katika Ukanda wa Ghaza kama ambavyo inapinga kuhujumiwa watu wasio na hatia nchini Yemen na pia kama ambavyo inapinga kukandamizwa watu wa Bahrain pia inapinga hatua ya Marekani kutumia ndege zisizo na rubani au drone dhidi ya wananchi wa Pakistan na Afghanistan.  Aidha amesisitiza kuwa, katika msingi wa mantiki ya wazi ya Imam Khomeini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inawaunga mkono watu wanaodhulumiwa na kuongeza kuwa: "Ni kwa sababu hii ndio Palestina ikawa kadhia kuu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kamwe nchi hii haitaacha kufuata sera hii." Katika sehemu nyengine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ametoa wito kwa Waislamu duniani kuchukua tahadhari ili wasitumbukie katika mtego wa maadui wanaoibua hitilafu miongoni mwa Waislamu.

captcha