
Katika Qur’ani Tukufu, mzizi mkuu wa neneo hili umekuja mara 234 kwa sura mbalimbali, na Qur'ani Tukufu imehimiza kuomba msamaha mara saba. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametajwa mara 91 kwa sifa ya Ghafūr (Mwenye kusamehe sana), mara tano kwa sifa ya, Ghaffār, (Mwenye kusamehe mara kwa mara), na mara moja kwa sifa ya Ghāfir (Mwenye kusamehe).
Upana wa maelezo haya kuhusu msamaha katika kushughulika na wenye dhambi unaonyesha wingi wa rehema na huruma ya Allah Subhānahu wa Ta‘ālā. Ingawa maghfira maana yake ni kufunika, kufunika kwa Allah hakufanani na msamaha wa binadamu. Mwanadamu akimsamehe mwenzake huacha kosa lake lakini athari ya dhambi hubaki moyoni na viungo vyake kama uchafu na najisi, kama Qur’ani inavyosema:
“Matendo yao yameweka pazia juu ya nyoyo zao.” (Surah al-Mutaffifīn, aya ya 14).
Lakini kufunika kwa Allah SWT maana yake ni kuondoa kabisa athari na matokeo ya dhambi. Hii ni daraja ya juu zaidi ya msamaha, na ni neema isiyo na kifani inayotoka kwa Muumba wa ulimwengu. Wakati mwingine, kufunika huku hufikia kiwango cha kubadilisha dhambi kuwa mema, kama Allah anavyosema kuhusu wale waliotenda madhambi makubwa na kustahiki adhabu mara mbili:
“…Isipokuwa yule anayejitubu, akawa na imani na akatenda mema; hao Allah atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allah daima ni Mwingi wa kusamehe na Mwenye rehema.”
(Surah al-Furqān, aya ya 70).
3495216