Katika miezi ya hivi karibuni, wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano karibu kila siku kwa ajili ya kulalamikia siasa za serikali za kuwatia nguvuni wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo, maandamano ambayo yamekuwa yakivunjwa na kukandamizwa na askari jeshi wa nchi hiyo pamoja na wale wa kivamizi wa Saudi Arabia. Kuhusu jambo hilo, Stephane Dujarric Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake juu ya hukumu iliyotolewa dhidi ya Sheikh Ali Salman na kutaka hukumu hiyo itazamwe upya. Akizungumza siku ya Jumatano, Stephane Dujarric alikosoa namna kesi ya Sheikh Salman ilivyoendeshwa kwa kusema haikuwa na uwazi na kusisitiza kwamba utawala wa Bahrain unapasa kuheshimu uhuru wa kujieleza pamoja na kuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara nchini. Siku ya Jumanne utawala huo ulimpa Sheilh Ali Salman kifungo cha miaka minne jela kwa kosa la eti kuwachochea wananchi waupindue utawala huo. Kutolewa kwa hukumu hiyo kumezua maandamano makubwa nchini Bahran na ukosoaji wa kimataifa dhidi ya utawala wa Aal Khalifa. Ukosoaji mkubwa wa Ulaya umefanywa na nchi za Ireland, Jamhuri ya Czech na Uswisi katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao cha baraza hilo huko Geneva, wawakilishi wa nchi hizo tatu walilaani vikali siasa za ukandamizaji zinazotekelezwa na utawala wa Bahrain dhidi ya wapinzani. Walisema siasa hizo zinazotumiwa kuwakandamiza wanasiasa na wanaharakati wanaopigania uhuru, demokrasia na utawala bora nchini humo si za kisheria.
Huku akizishukuru nchi hizo kwa kupinga siasa hizo za utawala wa Aal Khalifa, Jalal Firuz, mbunge wa zamani wa Bahrain amesisitiza kuwa licha ya kuwepo ukandamizaji huo, lakini wananchi wa Bahrain wataendelea kufanya maandamano ya amani hadi matakwa yao yote yatakapotekelezwa.
Tokea mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi ambao wanataka kufanyike marekebisho ya kisiasa, kiutawala na uchaguzi huru na wa kidemokrasia ambao utasaidia kuondolewa kwa ubaguzi wa kimadhehebu, kikabila na rangi nchini humo. Katika kukandamiza maandamano na malalamiko hayo ya wananchi wa Bahrain, askari jeshi wa nchi hiyo wakishirikiana na wa Saudi Arabia hadi sasa wamekwishawaua waandamanaji 150 na kuwajeruhi pamoja na kuwatia nguvuni mamia ya wengine.../mh