Wito huo umetolewa na Ayatullah Muhsin Araki Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ambaye amesisitiza umuhimu wa maulamaa Waislamu duniani kuzingatia kadhia ya Palestina. Katika barua aliyowaandikia maulamaa Waislamu duniani, Ayatullah Araki ametoa salamu zake za kheri na fanaka kwa mnasaba wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwataka washiriki katika hafla za Siku ya Kimataifa ya Quds. Katika barua yake hiyo, Ayatullah Araki amesema kadhia ya Palestina ni kadhia ya Umma wote wa Waislamu na nguzo ya Umoja wa Kiislamu.
Huku akibainisha masikitiko yake kuhusu ugaidi na jinai zinazotekelezwa na kundi la kitakfiri la Daesh au ISIS huko Iraq na Syria pamoja na hali mbaya ya Yemen sambamba na migogoro katika nchi zingine za Waislamu, amesema pamoja na hayo Waislamu hawapaswi kusahau kadhia ya Palestina. Ayatullah Araki ameelezea matumaini yake kuwa Umoja wa Kiislamu utabainika kwa mara nyingine katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa, Imam Khomeini MA, hayati mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, manmo Agosti mwaka 1979 alitangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds. Alitoa wito kwa Waislamu kote duniani kuiadhimisha siku hii kwa maandamano kote duniani kwa lengo la kushikamana na harakati za ukombozi wa Palestina na kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel uondoke katika ardhi unazokaliwa kwa mabavu za Palestina hasa Quds Tukufu. Mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Quds inatazamiwa kuwa Julai 10.../mh