IQNA

Dunia yawalaani Wazayuni waliomchoma moto mtoto wa Kipalestina

18:45 - August 01, 2015
Habari ID: 3337635
Kitendo cha kinyama cha Wazayuni wa Israel cha kumchoma moto hadi kufa mtoto mchanga wa Palestina mwenye umri wa miezi 18 kimeendelea kulaaniwa kote duniani.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imekilaani kitendo hicho kiovu na kubainisha kwamba, kinaonesha jinsi Wazayuni walivyobobea kwa ugaidi. Mufti Mkuu wa Misri Sheikh Shauqi Allam amelaani kitendo hicho cha walowezi wa Kiyahudi na kusisitiza kuwa, kitendo hicho cha kinyama kinakinzana na sheria zote za kimataifa pamoja na fitra na maumbile ya mwanadamu. Mufti Mkuu wa Misri amezitaka nchi za Kiarabu, Kiislamu na asasi za kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha jinai hizo za Wazayuni zinasitishwa mara moja. Riyadh Mansour, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ametoa wito kushtakiwa na kupandishwa kizimbani waliohusika na jinai za kumchoma moto mtoto mdogo wa Kipalestina. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon amelaani kitendo hicho cha Waisraeli na kukitaja kuwani ugaidi.
Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali kitendo kiovu cha Wazayuni wa Israel cha kumchoma moto hadi kufa mtoto mdogo wa Palestina.
Marziyeh Afkham amesema jinai hiyo ya Wazayuni inazihamasisha dhamira zilizo hai za walimwengu kufanya jitihada za kukomesha maafa hayo ya kutisha. Afkham amesema jinai hiyo imeonesha tena hakika na utambulisho wa utawala wa Kizayuni wa Israel na ukatili unaotawala jamii na siasa za utawala huo.
Asubuhi ya jana walowezi wa Kiyahudi walishambulia kijiji cha Duma katika Ukingo wa Magharibi na kuchoma moto nyumba mbili za Wapalestina. Wazayuni hao wamemchoma na kumuua mtoto mdogo aliyekuwa na umri wa miezi 18 kwa jina Ali Saad Dawabsha katika hujuma hiyo ya kinyama na kuwajeruhi vibaya wazazi na ndugu mwenye umri wa miaka minne wa mtoto huyo.../mh

3337207

captcha