IQNA

Usajili Wafunguliwa kwa Mashindano ya 21 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu Algeria

15:29 - October 25, 2025
Habari ID: 3481414
IQNA – Usajili umefunguliwa rasmi kwa toleo la 21 la Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu nchini Algeria, mojawapo ya mashindano yenye heshima kubwa katika kanda ya Afrika Kaskazini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Dini na Waqfu ya Algeria, maombi ya kushiriki katika awamu ya awali yatapokelewa kuanzia tarehe 20 hadi 31 Oktoba 2025. Usajili utafanyika pekee kupitia jukwaa rasmi: moussabaka.marw.dz.

Wizara imetangaza kuwa washiriki wanaweza kujisajili katika makundi matatu: Mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi na kusoma Qur’ani, mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi, kusoma, na kufasiri Qur’ani na kundi maalum kwa wahifadhi chipukizi walio chini ya umri wa miaka 15

Masharti ya umri ni kati ya miaka 15 hadi 25 kwa mashindano ya kimataifa, na chini ya miaka 25 kwa mashindano ya kitaifa.

Wale waliowahi kushinda nafasi tatu za juu kitaifa au kutambuliwa kama wasomaji wa kitaifa au kimataifa hawataruhusiwa kushiriki mwaka huu.

Wizara imeeleza kuwa lengo la mashindano haya ni “kuhamasisha uhifadhi wa Qur’ani Tukufu na kuibua vipaji vya kipekee vya Qur’ani kutoka mikoa mbalimbali ya Algeria,” sambamba na kuwaandaa washindi kuwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa yajayo.

Mashindano haya, yanayojulikana pia kama Tuzo ya Qur’ani ya Algeria, yalizinduliwa mwaka 2003 na tangu wakati huo yamevutia washiriki kutoka ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Toleo la 20 lililofanyika mwaka 2024 mjini Algiers liliwaleta pamoja qari kutoka zaidi ya nchi 44, ambapo tuzo kuu zilitolewa kwa washindi wa hifadhi na Tajweed (kanuni za usomaji wa Qur’ani). Kawaida, mashindano haya hufanyika katika mwezi wa Ramadhani chini ya udhamini wa Rais wa Algeria.

/3495128

Kishikizo: algeria qurani tukufu
captcha