IQNA

Tishio la Bomu Laisimamisha Shughuli za Msikiti wa Kilbirnie Nchini New Zealand

14:38 - October 25, 2025
Habari ID: 3481411
IQNA – Polisi nchini New Zealand wanafanya uchunguzi kuhusu tishio la bomu lililolenga Msikiti wa Kilbirnie uliopo Wellington, hali iliyosababisha kusitishwa kwa shughuli zote za msikiti huo kwa muda.

Maafisa wa usalama wamesema tishio hilo lilitumwa siku ya Alhamisi kupitia jukwaa la mtandaoni, na lilijumuisha anuani kamili ya Msikiti wa Kilbirnie.

Kituo cha Kiislamu cha Wellington kimethibitisha taarifa hiyo na kueleza kuwa misikiti mingine na vituo vya Kiislamu katika jiji hilo pia vimearifiwa kuhusu tishio hilo.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya Kiislamu nchini New Zealand (FIANZ), msikiti huo hupokea vitisho mara kwa mara. Mwenyekiti wa kamati ya utetezi wa FIANZ, Abdur Razzaq, ameieleza gazeti la Herald kuwa “mwitikio wa polisi umekuwa wa kuridhisha.”

Diwani Nureddin Abdurahman kutoka kata ya Kusini ya jiji hilo amesema alipokea barua pepe kutoka FIANZ kuhusu tishio hilo, na ameeleza kuwa mamlaka “zinachukua tahadhari stahiki.”

Polisi wameiambia Herald kuwa “hakuna tishio la moja kwa moja linalojulikana kwa jamii kwa sasa.”

New Zealand imekumbwa na changamoto kubwa zinazohusiana na chuki dhidi ya Uislamu na mashambulizi dhidi ya misikiti. Mnamo Machi 2019, waumini 51 waliuawa katika mashambulizi ya bunduki kwenye Msikiti wa Al Noor na Kituo cha Kiislamu cha Linwood huko Christchurch.

Tume ya kifalme iliyoundwa baadaye ilibaini kuwa Waislamu nchini New Zealand hukumbwa mara kwa mara na ubaguzi, kauli za vitisho, na kutoripoti matukio ya chuki kwa mamlaka husika.

3495135

Habari zinazohusiana
captcha