Ayatullah Khamenei ameyasema hayo Jumanne mjini katika mazungumzo na Rais Heinz Fischer wa Austria na ujumbe aliofuatana nao katika ziara yake rasmi nchini Iran.
“Hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya kutii kibubusa sera hasimu za Marekani kuhusu Iran ni kinyume cha mantiki,” amesema Kiongozi. Aidha ameipongeza Austria kwa kutofuata sera hizo za Marekani zisizo na mantiki wala msingi.
Ayatullah Khamenei amesema lengo kuu la Mapinduzi ya Kiislamu ni kudhamini kheri na saada kwa ajili ya wananchi wa Iran na wanadamu wote chini ya kivuli cha “kushikamana na njia ya Mwenyezi Mungu na kutawala akili na imani kunakoambatana na matendo” na akaongeza kuwa bila ya shaka mtazamo huu wenye nia ya kheri una maadui pia katika uga wa kimataifa ambao wanashupalia vita na kuyachonganisha mataifa; lakini Iran inao marafiki wengi wazuri na wa dhati miongoni mwa nchi na mataifa.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia uadui usio na mantiki wa baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na akasema: “Mapinduzi ya Kiislamu” yaliikomboa Iran ambayo ilikuwa chini ya mamlaka kamili ya Wamarekani, na suala hili ndio sababu ya uadui wa Marekani na Jamhuri ya Kiislamu”. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia vitendo na ufisadi unaofanywa na watu waliopotoka katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kutumia jina la Uislamu na kusisitiza kwamba Uislamu sio ule unaotangazwa na watu hao, bali Uislamu umesimama juu ya misingi imara ya mantiki, imani na akili.
Kiongozi Muadhamu aidha amesisitiza ulazima ulazima kwa viongozi wa Iran na Austria kuwa na mipango na ufatiliaji kwa ajili ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili.
Katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Iran, Rais Fischer wa Austria amebainisha furaha yake kufuatia mkutano wake na Kiongozi Muadhamu pamoja na mtazamo wake chanya kuhusu Austria. Ameongeza kuwa, “fursa mpya imeibuka katika kuimarisha uhusiano wa nchi mbili.”.../mh