Kwa mujibu wa tovuti ya dnaIndia, maulamaa 1,050 wakiwemo pia wakuu wa taasisi muhimu za Kiislamu India wamekutana kwa mara ya kwanza na kutoa Fatwa hiyo muhimu dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS.
Maulamaa na viongozi hao wa Waislamu India pia wamelaani vikali jinai na ukatili wa ISIS dhidi ya watu wasio kuwa na hatia duniani hasa Mashariki ya Kati.
Fatwa hiyo imeungwa mkono na tassisi 12 muhimu zaidi za Kiislamu India ikiwemo Jumuiya ya Maulamaa Bombay na Baraza Kuu la Maulamaa India. Sehemu ya Fatwa hiyo inasema: "Uislamu unapinga mabavu na ukatili katika hali ambayo ISISI daima wanatekeleza ukatili."
Katika Fatwa hiyo Mamufti na Maulamaa wametoa wito kwa madhehebu zote za Kiislamu India kulaani vitendo vya ISIS kwani kundi hilo lwa wakufurishaji limechafua sura ya Uislamu duniani.
Fatwa hiyo imetolewa baada ya kubainika kuwa kundi la ISIS linatekeza njama za kuwasajili vijana Waislamu India wajiunge na kundi hilo haramu la kigaidi. Nakala ya Fatwa hiyo imekabidhiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na vile vile wawakilishi wa nchi zaidi ya 50 ili kubainisha msimamo wa Maulamaa wa India kuhusu ugaidi.
Fatwa hiyo imetoa wito kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua zinazohitajika kuangamiza kundi hilo la kigaidi.../mh