Akizungumza kwenye halfa ya kijeshi ya kuanza rasmi wiki ya kujihami kutakatifu hapa nchini, Rais Rohani amesema “Kama tulivyowasaidia wananchi wa Iraq na Syria kupambana na magaidi kufuatia maombi ya serikali zao, ndivyo hivyo hivyo tutakavyofanya endapo nchi zingine majirani zitakumbwa na tatizo la ugaidi na kututaka msaada” Tarehe kama ya leo miaka 35 iliyopita, dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein aliivamia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada na uungaji mkono wa nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu na kuanzia hapo vikaanza vita vya miaka 8 vya kulazimishwa ambapo Iran ilitoa pigo kubwa kwa utawala vamizi wa Saddam. Akizungumzia vita hivyo, Rais Rohani amesema kuwa, wananchi wa Iran walionyesha umoja na mshikamano wa dhati dhidi ya wavamizi na mwisho wa siku wakapata ushindi.
Rais wa Iran amesema vita vya kulazimishwa katika muongo wa 80 vilionyesha wazi kuwa Iran haina sera ya kuvamia na kuvuruga mambo ya nchi nyingine lakini pia ilidhihirisha wazi kwamba, taifa hili linapovamiwa hutumia nguvu zake zote kujilinda na kujibu mapigo.../mh