Katika maandamano hayo ya Alhamisi usiku mjini Awamiyah, washiriki wamesema wataendelea kuandamana hadi hukumu hiyo ya kidhalimu ibatilishwe. Ikumbukwe kuwa Tarehe 25 mwezi Oktoba Mahakama Kuu ya Saudi Arabia ilithibitisha hukumu ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr Baqir An-Nimr; na hukumu hiyo sasa inasubiri idhini ya saini ya Mfalme wa nchi hiyo Salman bin Abdulaziz Al Saud kwa ajili ya kutekelezwa. Endapo mfalme huyo atatoa idhini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia inaweza kuchukua hatua ya kutekeleza hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr bila ya kutoa taarifa na indhari kabla. Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu ilimwandikia barua Kamishna Mkuuwa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Zeid Al Hussein kumtaka aushinikize utawala wa Aal Saud ufute mara moja hukumu ya kifo uliyotoa dhidi ya Alimu huyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon naye pia ameitaka Saudia isimamishe utekelezaji wa hukumu hiyo. Sheikh Nimr An-Nimr alitiwa nguvuni mwaka 2012 na kufunguliwa kesi ya kuhatarisha usalama wa utawala wa Aal Saudi kutokana na kutoa hotuba dhidi ya utawala huo na kutetea wafungwa wa kisiasa. Hata hivyo mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameyakana mashtaka hayo.