IQNA

Jeshi la Nigeria lamkamata kiongozi wa Mashia Nigeria, naibu wake auawa

19:57 - December 13, 2015
Habari ID: 3462774
Jeshi la Nigeria limemkamata kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo, Sheikh Ibrahim Zakzaky, baada ya kutekeleza hujuma nyumbani kwake kaskazini wa nchi hiyo.

Walioshuhudia wanasema idadi kubwa ya wanajeshi walishambulia na kuteketeza kwa moto sehemu kadhaa za nyumba ya Zakzaky kabla ya kumtia mbaroni Jumapili hii. Baadhi ya duru zinasema hadi sasa jeshi la Nigeria limeua zaidi ya Waislamu 70 wa madhehebu ya Shia tokea ghasia zilizoanza jana katika ukumbi wa kidini wa Husseiniya Baqiyatullah katika mji wa Zaria jimboni Kaduna.

Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema Naibu wa Sheik Zakzaky, Sheikh Mohammad Turi ameuawa kwa kupigwa risasi katika machafuko hayo.

Ripoti zinasema wanajeshi waliokuwa katika eneo hilo walianzisha uchokozi kwa kuwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa wakiadhimisha kuanza mwezi wa Rabiul Awwal. Jeshi la Nigeria limedai kuwa Waislamu katika eneo hilo waliusimamisha msafara wa Mkuu wa Jeshi la Nigeria Luteni Jenerali Tukur Yusuf Buratai kwa sababu Sheikh Zakzaki alikuwa anapanga kutoa hotuba katika kituo cha kidini. Wakuu wa Nigeria wamedai kuwa, Sheikh Zakzaky alikusudia kumuua mkuu wa jeshi, madai ambayo ameyakanusha kabisa. Katika mahojiano yake na Press TV, Sheikh al-Zakzaky amesema madai hayo ni ya uongo na kwamba wanajeshi waliingia nyumbani kwake na kufyatua risasi kiholela ambapo amesema watu 30 waliuawa papo hapo.

Watetezi wa haki za binadamu wameilaumu vikali serikali ya Nigeria kwa kukiuka haki za kidini na kijamii kwa kushambulia mijumuiko ya amani ya Mashia. Mwezi Julai mwaka jana karibu Waislamu 24 wa madhehebu ya Shia waliuawa baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds.

3462830

captcha