IQNA

Sala ya Jamaa ya pamoja ya Mashia na Masunni nchini Iraq

14:05 - January 23, 2016
Habari ID: 3470078
Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni Iraq katika wilaya ya Al Mikdadiya mkoani Diyala nchini Iraq wamesali pamoja sala ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Zayyid Al-Azzawi mkuu wilaya ya Al Mikdadiya jana Ijumaa alisema: "Masunni na Ahul Sunna katika eneo la Al Mikdadiya wameswali pamoja sala ya Jamaa katika Masjid La Ilaha ila Allah mjini Ashur, makao makuu ya wilaya.”

Al-Azzawi ameongeza kuwa lengo la kusaliwa sala hiyo ni kusisitiza umoja wa Waislamu na kukurubisha zaidi madhehebu za Kiislamu katika eneo hilo ili kukabiliana na wanaolenga kuibua fitina za kimadhehebu. Amebaini kuwa: "Maulamaa wa Ahlul Sunna na Shia ambao wameshiriki katika sala hiyo wametoa wito kwa Waislamu wa madhehebu zote kuishi pamoja kwa amani na kwamba ni haramu kumwaga damu ya ndugu Mwislamu.”

Naye Meja Jenerali Jassim Al Saadi mkuu wa polisi katika mkoa wa Diyala ambaye pia alishiriki katika sala hiyo alisisitiza kuwa kusaliwa sala hiyo ni ujumbe mzito kwa wenye kueneza fitina za kimadhehebu kwamba watu wa Al Mikdadiya watakabiliana nao.

Wiki iliyo pita kulishuhudiwa mapigano ya kimadhehebu huko Al Mikdadiya ambapo watu zaidi ya 70 walipoteza maisha.


3469319
captcha