IQNA

Chakula kinachotupwa Makka chaweza lisha mamilioni, Qur'ani yasemaje?

7:12 - January 25, 2016
Habari ID: 3470085
Israfu au kumwaga chakula kwenye jalala ni dhambi kubwa na adha ya kijamii. Kitendo hiki haramu leo kinadhihirika katika migahawa na dhifa mbali mbali katika mji Mtakatifu wa Makkah.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kiwango cha israfu ya chakula katika mji wa Makka pekee kinatosha kulisha asilimia 17 ya watoto wenye njaa katika nchi 18 zinazostawi duniani au kuwalisha mamilioni ya watu wenye njaa duniani.

Mkurugenzi wa mradi wa misaada ya chakula mjini Makka anasema hivi kuhusu israfu mjini humo: "Chakula kinachotupwa mjini Makka kinaweza kuwalisha watoto wengi wenye njaa Afrika, Asia na nchi za Amerika ya Latini."

Ahmad Al-Matrafi anaongeza kuwa: "Chakula kinachotupwa katika dhifa ya harusi ya kawaida mjini Makka kinatosha kuwalisha watu 250 wenye njaa."

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa kufuatia ongezeko la watu Saudi Arabia, chakula kinachotupwa kwenye mapipa ya takataka kitaongezeka kutoka tani milioni 14 mwaka huu hadi tani milioni 17.5 mwaka 2020. Chakula hicho kina weza kuwalisha watoto milioni 4.8 wenye njaa maeneo mbali mbali duniani.

Israfu hiyo ya chakula inajiri katika mji mtakatifu zaidi wa Kiislamu katika hali ambayo Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Kiislamu yamejaa maamurisho ya kujiepusha na israfu, kuwasaidia wasiojiwea na kuwalisha masikini. Hapa tutataja baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu kuhusiana na maudhui hii. Surat Taha aya ya 127, Allah SWT anasema: Na hivi ndivyo tutakavyo mlipa kila apitaye kiasi, na asiye amini ishara za Mola wake Mlezi. Na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi, na inadumu zaidi.

Halikadhalika katika Surat Al A'Raaf aya ya 31 Allah SWT anasema: " Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu.

Pia katika Surat Ghaafir sehemu ya aya ya 28 Allah SWT anasema. " …Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa"

3469737

captcha