Kampeni hiyo ambayo imezinduliwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inaongozwa na Mamlaka ya Jumla ya Usalama wa Chakula na ina inalenga kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa usalama wa chakula na kuhimiza watu wazingatia wastani katika matumizi ya chakula.
Takriban SR40 bilioni (dola bilioni 10.6) za chakula hupotea kila mwaka katika Ufalme wa Saudia, au karibu theluthi moja ya jumla ya chakula kinachotumiwa.
Ili kuendeleza kampeni hiyo mamlaka ilitoa video ya wavulana na wasichana wadogo wakijadili jinsi familia zao zilivyofanya israfu na kutupa chakula wakati wa Ramadhani.
Watoto hao walieleza jinsi meza zao zilivyokuwa zikifurika kila aina ya chakula na kueleza wasiwasi wao kuhusu upotevu huo. Familia zimetakiwa kutumia vyema chakula kilichobakia na kukitumia katika futari itakayofuata au kuhakikisha kuwa chochote ambacho hawahitaji kinatolewa kwa mtu ambaye anaweza kufaidika nacho.
Mamlaka hiyo ilisema kampeni hiyo ilivutia hisia za watu na ilikuwa ikisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.
Mwaka 2019, Saudi Arabia ilitangazwa kuwa nchi inayoongoza kati ya nchi 25 duniani zinazomwaga na kutupa jaani kiwango kikubwa zaidi cha chakula.
Kitengo cha wanataaluma wa masuala ya biashara cha jarida la The Economist, kimetangaza kuwa, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa, nchi 25 zinamiliki karibu asilimia 87 ya Jumla ya Pato la Dunia na kwamba Wasaudia wanaongoza kati ya raia wa nchi zote duniani katika israfu ya umwagaji na utupaji mabaki ya chakula.
Wakati huo, Wizara ya Mazingira, Maji na Kilimo ya Saudia ilitangaza kuwa kila raia mmoja wa nchi hiyo humwaga kilogramu 250 za chakula kwa mwaka, kulinganisha na wastani wa dunia wa kilo 115, Kitengo cha Wanataaluma cha The Economist kinasisitiza kuwa, kiwango halisi cha utupaji chakula unaofanywa na kila raia mmoja wa nchi hiyo ni kikubwa zaidi ya kiwango hicho rasmi kilichotangazwa na serikali ya Riyadh. Kwa mujibu wa kitengo hicho, kiwango hicho ni karibu kilo 427 za chakula kwa mwaka.
4130009