IQNA

Hujuma ya kigaidi msikitini Saudia, Watu kadhaa wauawa shahidi

22:23 - January 29, 2016
Habari ID: 3470096
Watu kadhaa wameuawa shahidi kufuatia hujuma ya bomu na ufyatuaji risasi katika msikiti mmoja mjini al-Ahsa, katika mkoa wa Mashariki nchini Saudi Arabia.

Imearifiwa kuwa waumini watano wameuawa shahidi na watu 10 pia wamejeruhiwa katika hujuma hizo ambazo ziliulenga Msikiti wa Imam Ridha AS katika mtaa wa Mahasen huko al-Ahsa.

Walioshuhudia wanasema hujuma hizo za kigaidi zilijiri wakati wa Sala ya Ijumaa katika msikiti huo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Aliyeshuhudia anasema kulikuwa na mlipuko wa bomu katika uwanja wa wazi wa msikiti huku gaidi mwingine mwenye bunduki ya rashasha akiingia ndani ya msikiti na kufyatua risasi kiholela. Gaidi huyo alikamatwa na vijana waliokuwa ndani ya msikiti na sasa yuko mikononi mwa polisi. Mwaka 2015 kulijiri hujuma mbili za kigaidi katika misikiti ya Waislamu wa Madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia ambapo kundi la kigaidi la ISIS au Daesh lilidai kuhusika.

Waislamu wa eneo la mashariki mwa Saudia, ambao aghalabu ni wa madhehebu ya Shia, wamekuwa wakiandamana kwa amani tokea mwaka 2011 wakilalamikia ubaguzi wa utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Saud.

3471071

captcha