IQNA

Sayyed Nasrallah alaani kuhujumiwa msikiti wa Imam Ridha AS Saudia

11:42 - January 30, 2016
Habari ID: 3470098
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah amelaani shambulio la kigaidi la jana Ijumaa dhidi ya msikiti mmoja nchini Saudi Arabia.

Watu watano waliuawa kufuatia hujuma ya bomu na ufyatuaji risasi katika msikiti huo ulioko mjini al-Ahsa, katika mkoa wa Mashariki nchini Saudi Arabia. Imearifiwa kuwa watu 10 pia wamejeruhiwa katika hujuma hizo ambazo ziliulenga Msikiti wa Imam Ridha AS katika mtaa wa Mahasen huko al-Ahsa.

Kwingineko katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya moja kwa moja kupitia televisheni ya Al Manar Ijumaa usiku, Sayyed Nasrallah amepuuzilia mbali madai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaingilia masuala ya ndani ya Lebanon, akisisitiza kuwa hakuna ushahidi wowote juu ya tuhuma hizo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema Iran haihusiki kivyoyvote na ombwe la uongozi linaloshuhudiwa kwa sasa nchini Lebanon na kwamba Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon unaweza kutatuliwa tu na wananchi wa nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa Hizbulah amesema madai kwamba Iran inaingilia masuala ya ndani ya Lebanon haya msingi wala mashiko na kuwa yanaenezwa kwa lengo la uchochezi. Sayyid Hassan Nasrullah amesema: "Uhusiano wetu na waitifaki wetu umejengwa juu ya misingi ya kuaminiana, ukweli na heshima.”

3471098

captcha