
Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo Jumatatu mjini Tehranwakati alipoonana na makamanda na maafisa wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa, lengo kuu la kambi ya adui ni kuyasahaulisha malengo hayo matukufu ili baadaye wabadilishe mienendo ya watu ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa, njama kuu za kambi kubwa ya wanaoitakia mabaya Jamhuri ya Kiislamu, ni kutaka kuizuia isiendelee na harakati zake za kufanikisha malengo yake matukufu na ya kuitia nguvu Iran za kuweza kusimama kidete zaidi katika kukabiliana na maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakosoa pia viongozi wa Marekani na kusema kuwa, viongozi wa nchi hiyo ni wajuba kiasi kwamba, wanafanya vitendo vya kinyama na kutisha kabisa na baadaye wanakuchekea, je, haibidi kuwa macho kikamilifu mbele ya adui kama huyu?
Aidha amesema, uchaguzi una maana ya kuhuisha nguvu za taifa na ni kutangaza upya utiifu kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa, lengo lake la kusisitizia mno suala la watu wote kujitokeza vilivyo kwenye uchaguzi ni kuiletea heshima nchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na ndio maana kushiriki kwenye jambo hilo muhimu ni faradhi kwa wananchi wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja sherehe za Bahman 22 (Februari 11) za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu wa Februari huu nchini kuwa ni sikukuu mbili zenye maana kubwa kwa taifa la Iran na kusisitiza kuwa, kujitokeza wananchi wote katika uchaguzi wa Februari 26 kutakuwa na maana ya kuingiza damu mpya ya kuziwekea kinga, nguvu za Iran na za Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha amewapongeza wananchi wa Iran kwa kushiriki kwa wingi kwenye maadhimisho ya Bahman 22 yaani Februari 11 na kuongeza kuwa, mwaka huu pia wananchi watajitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho ya miaka 37 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kwa kujitokeza kwao huko kwa wingi, watazidi kumvunja moyo adui na kila mtu anayelitakia mabaya taifa hili.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, inabidi tukio hilo la Bahman 22 lidumishwe na lisisahauliwe hata kidogo na kusisitiza kuwa: Inabidi uhakika wa Mapinduzi ya Kiislamu ubakie daima katika nyoyo za watu hasa kwa kuzingatia kuwa mapinduzi hayo ndio kwanza yako katikati ya njia na kwa ajili ya kuimarisha misingi yake na kufikia kwenye malengo yake matukufu, yanahitajia kubakia hai katika malengo yake makuu.