Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo alasiri ya leo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Rais John Dramani Mahama pamoja na ujumbe wa ngazi za juu aliofuatana nao na kusisitiza kwamba, daima Iran imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha kwamba, kadhia ya Syria inamalizika kwa maslahi ya taifa la nchi hiyo na inaamini kwamba, nchi fulani kutoka nje haiwezi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa taifa hilo.
Ayatullh Khamenei amebainisha kwamba, Wamarekani na watu wa Ulaya hawawezi kuliainisha mambo taifa la Syria bali wananchi wa nchi hiyo wenyewe ndio wanaopaswa kuchukua maamuzi kuhusiana na mustakbali wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji kwamba, ni vipi magaidi wanapata fedha na silaha nyingi za kisasa na kuongeza kuwa, chimbuko la matatizo yote ni madola ya Uistikbari ambapo kinara wake ni Marekani na kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel ni dhihirisho la ushari.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, ufumbuzi wa suala la Syria na kukabiliana na matatizo kama ya ugaidi na masaibu ya wananchi wa Palestina unafungamana na kuweko ushirikiano zaidi wa nchi zenye kujitegemea.
Kiongozi Muadhamu ameashiria mtazamo chanya wa Iran katika kupanua ushirikiano na nchi za Kiafrika tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha kuwa, madola ya kibeberu yanapinga kuweko uhusiano mzuri kati ya Iran na Afrika na kwamba, madola hayo yamekuwa sababu kuu ya vita, machafuko na ndio ambayo yanayasaidia makundi ya kigaidi.