
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Sheikh Jalaalud-Din Sa'ab, aliyekuwa Imamu wa msikiti wa Jamia wa Rochdale aliuawa siku ya Alhamisi.
Inaelezwa kuwa, sheikh huyo mwenye asili ya Bangladesh alipoteza maisha baada ya kupigwa vikali na watu wasiojulikana wakati akielekea nyumbani kwa rafiki yake baada ya kumaliza kusali sala ya Ishaa kwenye msikiti huo.
Habari zaidi zimebaini kuwa, Sheikh Sa'ab alikumbwa na tukio hilo wakati watu wakipita na kuishia kushuhudia tu bila kutoa msaada wowote. Baada ya tukio hilo, sheikh huyo alikimbizwa hospitali ambako alipoteza maisha muda mfupi baadaye. Tayari polisi wameanzisha uchunguzi kwa ajili ya kubaini chanzo cha kifo cha sheikh Jalaalud-Din Sa'ab.
Aidha polisi ya mji huo imetangaza kumtia mbaroni mtu mwenye umri wa miaka 31 kwa kuhusika na mauaji hayo, ingawa hakuna taarifa kamili iliyotolewa kuhusu iwapo mtu huyo ana mahusiano na kundi lolote lenye chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza au la.
Wakati huo huo, Muhammad Shafiq, afisa mkuu mtendaji wa taasisi ya Ramadhan nchini Uingereza, amelielezea tukio hilo kuwa la kutisha na ameitaka serikali kuweka ulinzi katika maeneo yote yaliyo kando na misikiti ili kuzuia kujikariri vitendo kama hivyo.
Licha ya kwamba hadi sasa hakujatolewa ripoti kamili juu ya wahusika wa jinai hiyo, lakini weledi wa mambo wameihusisha na ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza baada ya tukio la kigaidi nchini Ufaransa.
Hivi karibuni kamisheni ya haki za binaadamu nchini Uingereza ilitoa ripoti kuhusu hali mbaya ya jamii ya Waislamu nchini humo na kuonyesha wasi wasi wake juu ya kuongezeka kwa wimbi la chuki dhidi yao.
3476820