IQNA

Iran yaionya na kuilaani vikali Bahrain kwa kumvua uraia Ayatullah Isa Qassim

12:20 - June 21, 2016
Habari ID: 3470405
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa kulaani hatua ya Bahrain ya kumvua uraia Ayatullah Isa Qassim.

Taarifa hiyo imelaani vitendo vya utawala wa kifalme wa Bahrain kukandamiza viongozi wa kidini na kitaifa nchini humo samamba na kuzuia uhuru wa kuabudu na kupora mali za waqfu za Wabahrain.

Wakati huo huo kufuatia hatua hiyo ya utawala wa Bahrain kumvua uraia mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Isa Qassim, kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameuonya vikali utawala wa Aal Khalifa

Katika taarifa siku ya Jumatatu, Jenerali Qassim Soleimani amesema: " Utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukiwadhulumu wananchi Waislamu wa Bahrain kwa muda mrefu mbali na kuwadhalilisha, kuwakandamiza na kuwatendea vitendo vilivyo kinyume cha ubinadamu na visivyo kubalika."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wananchi wenye subira wa Bahrain, wamekuwa wakiandamana kwa amani pamoja na kuwepo mashinikizo makubwa na ubaguzi wanaotendewa na utawala wa Aal Khalifa. Amesema pamoja na hayo, Wabahrain kamwe hawawezi kuondoka katika mkondo wao wa kutetea haki. Jenerali Soleimani amesema hivi sasa utawala wa Aal Khalifa unatumia kimya cha jamii ya kimataifa, Marekani na madola ya Magharibi kueneza ukatili wake dhidi ya watu wa Bahrain. Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kukiukwa haki binafsi za Ayatullah Isa Qasim ni mstari mwekundu na kwamba jambo hilo litawasha moto nchini Bahrain na kote katika eneo na wananchi kutokuwa na chaguo jingine isipokuwa kuanzisha mapambano ya silaha.

Siku ya Jumatatu, Utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa wa Bahrain ulitangaza kumvua uraia mwanazuoni mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu nchini humo Ayatullah Isa Qasim kwa madai kuwa emetumia vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.

3509030

captcha