IQNA

Hannaneh, ‘Kompyuta ya Kiirani’ katika mashindano ya Qur’ani Dubai

18:38 - November 11, 2016
Habari ID: 3470668
IQNA-Gazeti moja la Misri limemtaja Binti Muirani mwenye umri wa miaka tisa kuwa ‘kompyuta’ kutokana na ustadi wake katika kuhifadhi Qur’ani Tukufu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, tovuti ya habari Misri la ‘Al Masdar 7’ (source-7), imemtaja Hannaneh Khalfi binti Muirani mwenye umri wa miaka tisa kuwa ni ‘Kompyuta ya Kiirani’ kutokana na ustadi wake katika kujibu maswali wakati wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Sheikha Fatima Bint Mubarak yanayoendelea mjini Dubai.

Gazeti hilo limeandika kuwa Hannaneh ana kipaji cha kipekee kutokana na namna alivyohifadhi Qur’ani tukufu pamoja na uwezo wake wa kuainisha iwapo Sura iliteremka Makka au Madina. Tovuti ya ‘Al Masdar 7’ imeandika kuwa Hannaneh pamoja na mwakilishi wa Norway ni kati ya wanaoweza kupata nafasi ya kwanza katika mashindano. Jumatano Hannaneh Khalfi ambaye ni mshiriki mwenye umri wa chini zaidi katika mashindano hayo alijibu maswali ya majaji katika vikao viwili vya mashindano. Siku ya Alhamisi washiriki kutoka Algeria, Marekani, Qatar, Kenya, Ghana na Jamhuri ya Azerbaijan walipandaa jukwaa kuulizwa maswali.

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Sheikha Fatima Bint Mubarak yameanza Novemba 6 na yataendelea hadi Novemba 18 mjini Dubai. Kuna washiriki 70 wa kike waliohifadhi Qur’ani kutoka nchi 72 za Kiarabu, Afrika, Amerika ya Latini, Asia na Ulaya ambao watashiriki katika mashindano hayo ya kuhifadhi Qur’ani maalumu kwa wanawake.

Washiriki ni kutoka umri wa miaka 9 hadi 23 ambapo washindi wa nafasi za kwanza, pili na tatu watapata zawadi za fedha taslimu AED 250,000; AED 200,000; na AED 150,000 kwa taratibu.

Mashindano hayo ni sehemu ya mashindano ya Qur’ani yajulikanayo kama Zwadi ya Kimatiafa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai ambayo hufanyika kila mwaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

3545019

captcha