IQNA

Tafsiri ya Qurani kwa lugha ya ishara yazinduliwa Sharjah, Imarati

20:56 - November 12, 2016
Habari ID: 3470672
IQNA-Tafsiri ya Qur’ani Tukufu ya lugha ya ishara kwa ajili ya viziwi imezinduliwa katika Maonyesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Sharjah katika Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati)

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, tafsiri hiyo ya lugha ya ishara imewasilishwa kwa njia ya DVD. Mjumuiko huo una DVD 15 zenye masaa 60 ya tafsiri kwa lugha hiyo inayotumiwa na wale wenye matatizo ya kusikia na kuzungumza.

Shirika lililotegeneza DVD hizo limesema limetegemea tafsiri maarufu za Qur’ani katika nchi za Kiislamu na kwamba mbinu sahali na zenye kufikisha ujumbe viziru zimetumika.

Tafsiri hiyo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza nchini Jordan mwezi Februari mwaka 2011. Akizungumza wakati huo, Naibu Mkuu Jumuiya ya Kulinda Qur'ani ya Jordan Mohammad Khazar al Majali alisema mradi huo ulikamilika baada ya juhudi za miaka mitano kwa wenye matatizo ya kusikia.
Amesema mradi huo ulianza baada ya kuchapishwa msahafu kwa Braille kwa ajili ya wenye ulemavu wa macho.

Tafsiri hiyo imezinduliwa katika kibanda cha Jumuiya ya Kuilinda Qur’ani ya Jordan. Maonyesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Sharjah yalianza Novemba 2 na yamemalizika Jumamosi Novemba 12.

3545033

captcha