IQNA

Waislamu Algeria wapongeza fatua ya Ayatullah Khamenei kuhusu masahaba wa Mtume SAW

8:54 - June 27, 2018
Habari ID: 3471574
TEHRAN (IQNA)- Baraza Kuu la Kiislamu la Algeria limepongeza fatua iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei inayoharamisha kuwavunjia heshima masahaba wa Mtume SAW na ulazima wa kulinda heshima ya wake wa mtukufu huyo.

Baraza Kuu la Kiislamu la Algeria limeitaja fatua hiyo kuwa ni hatua muhimu katika mkakati wa kuimarisha umoja katika Umma wa Kiislamu.

Katibu Mkuu wa baraza hilo, Profesa Bouzid Boumediene amesema kuwa, matusi na vitendo vya kuwavunjia heshima watu vinasababisha ghasia na machafuko na kwamba baadhi ya kanali za televisheni za satalaiti zinachangia katika vitendo kama hivyo.

Katibu Mkuu wa Baraza la Kiislamu nchini Algeria amesisitiza kuwa, kuna ulazima wa kubuniwa sheria zinazokataza na kupiga marufuku kuchezea shere itikadi za kidini na kuvunjia heshima itikadi za watu kwani baadhi ya nchi zinachochea mivutano ya kimadhehebu kwa malengo yao ya kisiasa.

Ayatullah Ali Khamenei amekuwa akitahadharisha sana kuhusu njama za maadui za kutaka kuzusha hitilafu na mifarakano katika Umma wa Kiislamu na kuwataka Waislamu kuwa macho kuhusu taathira mbaya za njama hizo.

Fatua ya Ayatullah Khamenei ya kuharamisha vitendo na harakati zote za kuwavunjia heshima wake wa Mtume Muhammad SAW pia imetolewa katika mkondo huo.

Ayatullah Khamenei, akiwa ni Marjaa-Taqlidi wa Kishia ametoa fatua hiyo ya kudumu na ya kihistoria ambayo imetokana na jawabu yake kwa suali aliloulizwa na maulamaa wa Kishia wa nchini Saudi Arabia ambao walitaka kujua hukumu ya kumtusi na kumvunjia heshima Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Katika fatua yake hiyo, Ayatullah Khamenei anasema: "Kuzivunjia heshima nembo za ndugu zetu wa Ahlu Sunnah ikiwemo kumzushia tuhuma mke wa Mtume (bibi Aisha) ni haramu. Suala hili linajumuisha wake wa Mitume wote hususan Bwana wa Manabii, Mtume mtukufu Muhammad SAW."

Fatua hii imepokelewa vizuri sana na kwa wingi katika Ulimwengu wa Kiislamu ikiwemo Chuo Kikuu cha kidini cha Al-Azhar cha Misri, vyuo vikuu vya nchi za Kiarabu pamoja na shakhsia mashuhuri wa Kiislamu wa kila pembe ya dunia na hivyo kuhitimisha na kuzima moto wa kuzusha machafuko ya kimadhehebu katika jamii za Kiislamu.

Kumekuwepo na kanali za televisheni zinazodai kuwa ni za Waislamu wa madhehebu ya Shia ambazo aghalabu ziko mjini London Uingereza na zimekuwa zikiibua mifarakano katika umma wa Kiislamu kwa kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu  wa Ahul Sunna. Kuhusiana na kanali hizo, katika moja ya hotuba zake mwaka 2015, Ayatullah Khamenei alisema: "Kukabiliana na siasa za kuzusha mifarakano za Marekani na vituo vya kuzusha hitilafu ni miongoni mwa siasa za kimsingi za Iran. Ushia ambao kituo chake cha matangazo kiko London na kazi yake ni kuutayarishia njia ubeberu, sisi hatuutambui kuwa ni Ushia."

3725416

captcha