IQNA

OIC yalaani mpango wa katuni za kuuvunjia heshima Uislamu nchini Uholanzi

9:22 - August 30, 2018
Habari ID: 3471653
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani mpango wa kufanyika maonyesho ya katuni zenye kuvunjia heshima matukufu ya Uislamu nchini Uholanzi.

Tume Huru ya Kudumu ya Haki za Binadamu ya OIC imemlaani mwanasiasa wa Uholanzi mwenye chuki dhidi ya Uislamu, Geert Wilders wa chama cha mrengo wa kulia cha Freedom Pary, ambaye ametangaza mpango wa kuandaa mashindano ya katuni zenye kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad al Mustafa SAW.

Taarifa hiyo ya OIC imetoa wito kwa serikali ya Uholanzi kuchukua hatua za kupiga marufuku mashindano hayo.

OIC imetahadharisha kuwa hatua kama hiyo itachochea machafuko na kueneza utamaduni mbovu wa chuki mbali na kuumiza hisia za Waislamu zaidi ya bilioni 1.6 duniani.

OIC imeashiria Kipengee cha 19 cha Azimio la Ulimwengu la  Haki za Binadamu na pia Mkataba wa Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa na kusema  uhuru wa maoni una vizingiti na haki za wengine pia  zinapaswa kulindwa.

Wilders ni maarufu kwa misimamo yake ya chuki na kufurutu adha dhidi ya Uislamu na amewahi kuamsha hasira za Waislamu duniani kwa kutegeneza filamu iliyouvunjia heshima Uislamu. Hivi sasa anaishi chini ya ulinzi mkali baada ya tishio kwa maisha yake.

Mwaka 2016, mbunge huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Uholanzi alipatikana na hatia ya kuwatusi watu wenye asili ya Morocco na kuwabagua kwa misingi ya dini zao.

Wilders amewahi kusema huko nyuma kuwa, iwapo atafanikiwa kuwa Waziri Mkuu wa Uholanzi, atapiga marufuku Qur'ani Tukufu na kufunga misikiti yote nchini humo.

Kabla ya hapo Geert Wilders alikifananisha kitabu hicho cha mbinguni na kitabu cha 'Vita Vyangu' kilichoandikwa na Adolf Hitler.

Chama cha mwanasiasa huyo chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, kinaendelea kupata umashuhuri nchini Uholanzi kutokana na kujikita kwenye hisia za chuki dhidi ya wageni na Waislamu nchini humo na kote barani Ulaya.

Februari mwaka huu na katika kuendeleza vitendo vya unyanyasaji na chuki dhidi ya Waislamu, watu wenye chuki za kidini waliuchoma moto msikiti mmoja katika mji wa Drachten wa kaskazini mwa Uholanzi.

3466646

captcha