IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
19:38 - November 03, 2018
News ID: 3471727
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kudidimia nguvu na uwezo wa Marekani ni ukweli ambao wataalamu duniani wameafiki.

Ameongeza kuwa, "Taifa la Iran litakuwa na mustakabali bora na unaongaa kutokana na motisha, mori na jitihada za vijana."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran katika mkesha wa Tarehe 13 Aban ambayo ni Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu. Katika mkutano wake na maelfu ya wanafunzi na wanachuo, Kiongozi Muadhamu ameashiria suala la kufeli 'Shetani Mkubwa' (Marekani) katika njama zake za miaka 40 iliyopita dhidi ya Iran na kusema: "Kuzingirwa pango la ujasusi (ubalozi) la Marekani mjini Tehran mikononi mwa wanafunzi lilikuwa pigo kubwa la wanafunzi wa Iran kwa Marekani."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kukiri idadi kubwa ya wanasiasa na wataalamu wa jamii duniani kuhusu kuchakaa na kusambaratika 'nguvu laini' za Marekani na kusema kuwa: "Nguvu laini ya Marekani' inamaanisha kuzilazimisha nchi zingine zikubali mitazamo yake  na sasa iko katika hali dhaifu zaidi. Tangu alipoingia madarakani rais wa sasa wa Marekani mataifa mbalimbali hata yale ya Ulaya na pia China, Russia, India, Afrika na Amerika ya Latini yanapinga waziwazi maamuzi ya Marekani."

Ayatullah Khamenei amezitaka nchi za eneo la Mashariki ya Kati zizingatie ukweli kuhusu suala la kufifia uwezo wa Marekani na kusema: "Wale ambao kutokana na himaya ya Marekani wako tayari kusahau kabisa kadhia ya Palestina waelewe kuwa, uwezo wa Marekani unafifia hata katika eneo lake yenyewe na mataifa mbalimbali sasa yamejua ukweli na yameamka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema lengo la Marekani katika vita na vikwazo vyake vya kiuchumi katika muda wa miaka 40 iliyopita dhidi ya Iran lilikuwa kulemaza na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ibaki nyuma. Ameendelea kusema kuwa: "Matokeo ya vita hivyo vya kiuchumi yamekuwa kinyume na matakwa ya Marekani kwani taifa la Iran limechukua hatua ya kuelekea katika kujitegemea na uzalishaji wa ndani ya nchi, na mchakato huo umesonga mbele kwa kasi ambapo leo mamilia ya makundi ya vijana wataalamu katika vyuo vikuu wanajishughulisha na kazi muhimu ndani ya nchi."

Akijibu swali kuhusu kusimama kidete na kwamba uhasama wa taifa la Iran na Marekani utaendelea hadi lini, Ayatullah Khamenei amesema: "Pale Marekani itakapositisha ubeberu wake itawezekana kuamiliana nayo kama nchi zingine lakini hilo ni jambo lisolowezekana kwani dhati ya uistikbari ni kueneza ubeberu na satwa."

Kiongozi Muadhamu amesema hii leo nchi pekee duniani ambako Marekani haina nafasi hata kidogo katika maamuzi yake ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nukta hiyo ina maana kuwa Marekani imefeli kufikia malengo yake.

3760713

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: