IQNA

21:47 - April 12, 2019
News ID: 3471912
TEHRAN (IQNA) - Wananchi wa Iran wamejitokeza kote nchini baada ya Sala ya Ijumaa kuandamana kwa lengo kuonyesha uungaji mkono wao kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC na kulaani Marekani.

Maandamano hayo yamefanyika katika takriban miji yote mikubwa ya nchi, ukiwemo mji mkuu Tehran. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango na maberamu yenye jumbe za kuliunga mkono na kulipongeza jeshi la IRGC.

Aidha waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Israel'.

Siku ya Jumatatu, utawala wa Marekani ulitangaza kuliweka Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha yake ya makundi ya kigaidi. Uamuzi huo umechukuliwa ikiwa ni katika kuendeleza uhasama dhidi ya Iran na ni mashinikizo dhidi ya vikosi ambavyo, kwa kupambana na makundi ya kigaidi, vimefelisha  stratijia ya Washington katika eneo.

Kufuatia uhasama huo wa Marekani, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa, wanajeshi wote wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) na vikosi vyote vinavyofungamana nao ni kundi la kigaidi.

Wakati huo huo, Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, hatua ya Washington ya kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC katika orodha yake ya makundi ya kigaidi ni ya kipumbavu na kwamba Marekani ndiye mama wa ugaidi duniani.

Ayatullah Mohammad Ali Movahedi-Kermani ameyasema hayo leo hapa mjini Tehran katika hotuba za Sala ya Ijumaa huku akiwa amevalia sare rasmi za IRGC na kuongeza kwamba, kukipachika jina la ugaidi kikosi miongoni mwa vikosi vya jeshi la nchi yeyote ile kunakiuka sheria zote za kimataifa.

Amemuonya vikali Rais Donald Trump kuwa asijaribu kucheza na mkia wa simba, kwa kuwa IRGC inaweza kuigeuza Tel Aviv kuwa vifusi na majivu kwa makombora yake iwapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ataliruhusu kufanya hivyo.

Amemtaja Rais Donald Trump wa Marekani kama mtu mpumbavu ambaye hajui kile anachokifanya. Amebainisha kwamba Rais Donald Trump wa Marekani amechukua hatua ya kijinga kwa kuliweka jeshi la IRGC katika orodha yake na makundi ya kigaidi, na kwamba kitendo hicho kimekosolewa na hata Wamarekani wenyewe.

Amesema, "Wamarekani wenyewe wanatambua kuwa hatua hiyo ya Trump ilikuwa ya kipumbavu. Wachambuzi wa mambo wa Marekani wameonya kuwa, kitendo hicho cha Trump kitawaweka katika kipindi kigumu wanajeshi wa Marekani walioko katika eneo hili."

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa, kufeli kwa njama za Washington katika eneo hili la Asia Magharibi kumeighadhabisha mno nchi hiyo ya kibeberu, na ndio maana imewaelekezea hasira zake raia wa Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.

Ayatullah Movahedi-Kermani ameongeza kwamba, "Dunia nzima, hususan mataifa ya eneo hili yanafahamu fika kuwa Marekani ndiye mama wa ugaidi duniani. Marekani inafahamu vyema kuwa wao ndio waliolizalisha kundi la kigaidi la Taliban. Trump binafsi huko nyuma alikiri kuwa Marekani ndiye mwasisi wa ugaidi Asia Magharibi (Mashariki ya Kati)."

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa, taifa la Iran na makundi ya kisiasa licha ya mirengo yao ya kisiasa na tofauti zao za kimtazamo, lakini kwa sauti moja wanaliunga mkono Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC na kwa pamoja wanapinga hatua hiyo ya Trump.

3802972

Wananchi wa Iran waandamana kuunga mkono Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Name:
Email:
* Comment: